Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Mussa Manjaule akitoa taarifa ya minada ya mbaazi kwa msimu wa kilimo 2024/2025.
…………..
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
CHAMA Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCU LTD) katika msimu wa kilimo 2024/2025 kimekusanya na kuuza jumla ya tani 17,490 za mbaazi zilizowaingizia wakulima zaidi ya Sh.bilioni 12,452,649 katika minada tisa iliyofanyika kwenye vyama mbalimbali vya Msingi vya Ushirika(Amcos)Wilayani humo.
Mwenyekiti wa TAMCU Mussa Manjaule amesema,katika msimu wa 2024/2025 wamefanya jumla ya minada 9 iliyofanyika kwa mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania(TMX) ambao unamlinda mkulima kwa kupokea malipo yake moja kwa moja kutoka Chama Kikuu, badala ya utaratibu wa awali ambao wakulima walikuwa wanalipwa na Vyama vya Msingi vya Ushirika.
Alisema, fedha hizo zimekwenda kwa wakulima, Halmashauri ya Wilaya,vyama vya ushirika,waendesha maghala,wasafirishaji na wadau wengine waliopo kwenye mnyonyoro wa zao la mbaazi.
Aidha Manjaule alisema,katika msimu 2024/2025 uzalishaji wa mbaazi ni mkubwa tofauti na msimu 2023/2024 ambao walizalisha tani 9,na uzalishaji wa zao hilo unazidi kuongezeka mwaka hadi baada ya wakulima kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri.
Manjaule ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania,amewashukuru wakulima kutokana na jitihada wanazofanya mashambani,na ameomba waendelee na kilimo cha mbaazi kwani mkakati wa TAMCU kuwa na mazao matatu ya biashara ambayo ni korosho, mbaazi na ufuta.
“Tulianza na zao la ufuta na wakulima walipata fedha nyingi sana,sasa tunamalizia zao la mbaazi kwa kuwalipa wakulima wetu,baada ya hapa tunakwenda kwenye zao la korosho,mazao haya yanawafanya wakulima katika Wilaya yetu kupata fedha wakati wote”alisema Manjaule.
Alisema katika msimu huu soko la mbaazi limeyumba kwani bei ilikuwa Sh. 620 na Sh.710 tofauti na msimu uliopita ambapo bei ilikuwa Sh.800 hadi 1,200 kwa kilo moja ambapo amewasisitiza wakulima,wasikate tamaa kutokana na bei kushuka,badala yake waendelee kulima zao hilo.
Afisa ushirika kutoka Tume ya maendeleo ya Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Raymond Raphael,amewashauri wakulima wilayani Tunduru kulima mazao mchanganyiko ili kujiongezea kipato.
Raymond alisema wakati wanaelekea kwenye msimu mpya wa korosho ni vyema wakulima wazingatie suala la ubora na kuuza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao mkulima ana uhakika wa soko na bei nzuri.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake,Mkulima kutoka Chama cha Msingi Namsosa kata ya Namakambale Nurdin Chakilo alisema,minada ya mbaazi imekwenda vizuri kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Chakilo alisema mfumo wa stakabadhi ghalani una manufaa makubwa kwani mkulima analipwa fedha zake kwa wakati na kumwezesha kuendelea na shughuli za maandalizi ya msimu mpya wa kilimo.
“Ombi letu kwa Serikali ifanye jitihada za kuongeza bei ya mazao kama inaweza ili tuweze kulima kwa tija,bei yam waka huu sio mbaya sana,lakini kama msimu ujao itaongezeka basi itakuwa faraja kubwa kwetu wakulima.
Chakilo, ameiomba Serikali kuongeza nguvu kwenye kilimo kwa kutoa mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji wa zao hilo la mbaazi,ufuta na korosho hasa wakati huu ambao kilimo ni nguzo kubwa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja,vyama vya ushirika na Taifa.







