NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) Kata ya Chanika kimeibuka na ajenda ya kuimarisha miundombinu ya shule na uwezo wa kiuchumi kwa wanawake, baada ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha Haki za Uongozi na Uchumi kwa Wasichana na Wanawake pamoja na Wenye Ulemavu (WLER) yanayoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na UN Women.
Kupitia utekelezaji wa mradi huo wananchi wameungana na viongozi wao katika kuhakikisha shule za kata hiyo zinakuwa na vyumba maalumu vya kujisitiri watoto wa kike, hususan waliopo kwenye mazingira hatarishi na wenye ulemavu, pamoja na kutoa elimu ya mikopo kwa wanawake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa KC Chanika, Bi. Tatu Sultan, amesema kupitia mradi huu wamepata uelewa mpana uliowapelekea kudai vyoo rafiki hasa kwa. watoto wa kike baada ya kuelewa umuhimu wa kuwa na vyoo salama ambavyo vinakidhi mahitaji ya wasichana.
“Tulipata nafasi ya kujitambulisha katika serikali za mitaa na kufanya ufuatiliaji. Tulikuta miundombinu ya vyoo sio rafiki, hasa kwa watoto wa kike wenye ulemavu. Pia tulibaini uhaba wa taulo za kike,” alisema Bi. Tatu.
Amesema katika masuala ya uchumi, wameelewa na watawaelimisha na kuhamasisha wanawake wenzao kujishughulisha na kazi zinazowaingizia kipato
“Serikali inatoa elimu ya namna ya kukopa, lakini wakopaji wengi wana uelewa mdogo. Tamaa inatangulia kuliko maarifa,” amesisitiza.
Bi. Tatu amesema baadhi ya shule tayari zimepiga hatua na kupata vyumba vya kujisitiri wasichana, na lengo ni kufikia asilimia 50 ya shule za kata hiyo ifikapo mwaka 2026.
Kwa upande wake, mdau wa masuala ya kijinsia wa kata hiyo, Bi. Nifaeli John, amesema wamefanya kampeni za nyumba kwa nyumba na shuleni, wakitoa elimu kuhusu afya ya uzazi, mimba za utotoni na namna ya kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia.
“Baadhi ya wanawake na watoto wametuelewa. Wanatufuata kupata elimu zaidi, na wengine wametamani kujiunga na vikundi vya ujasiriamali,” amesema.
Licha ya hatua chanya zinazofikiwa nchini ikiwemo kupata Rais mwanamke kwa mara ya kwanza wanawake wengi bado wanakabiliwa na changamoto za mfumo dume, umaskini na mila kandamizi, zikiwemo ndoa na mimba za utotoni zinazopunguza fursa za kielimu na kiuchumi kwa wasichana.
Kwenye masuala ya upangaji wa bajeti jamii imekuwa na uwezo wa kutambua, kupanga na kuwasilisha masuala muhimu ya jamii. Mradi huu umekuza ushirikiano kati ya kituo cha taarifa na maarifa na viongozi wa serikali ya mtaa ili kushughulikia changamoto za kijamii pamoja mfano. Kesi za ukatili wa kijinsia
Baada ya mafunzo Wanawake wamejitambua na kushiriki kwenye vikundi vya kijamii ili kujenga ushirikiano wa kupata Fedha, kuanzisha Miradi ya pamoja
Mradi wa WLER umeendelea kujikita katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, kuibua viongozi wanawake ngazi za jamii, na kubadilisha mitazamo kandamizi ili wanawake washiriki kikamilifu kwenye maamuzi na uchumi.

















