Moja ya Picha zilizopigwa kabla ya kuuzwa kituo cha Mafuta cha Moshi Oil.
Mwananchi wa Jiji la Dar es Salaam Kata ya Kivule Mtaa wa Kipunguni B, Paschal Paul Niboye, maarufu kama Mzee Moshi Bar akizungumza jana Oktoba 24, 2025 na waandishi wa habari.
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MWANANCHI wa Jiji la Dar es Salaam Kata ya Kivule Mtaa wa Kipunguni B, Paschal Paul Niboye, maarufu kama Mzee Moshi Bar, ameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuingilia kati sakata la mali zake kuuzwa na Benki ya Equity bila kufuata taratibu za kisheria, akidai hajashindwa kulipa deni lake na ana uwezo wa kufanya marejesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Oktoba 24, 2025 Niboye alisema alianza mradi wa ujenzi wa kituo cha mafuta (sheli) kupitia mkopo alioupata kutoka benki hiyo, lakini kabla ya kukamilisha ujenzi alianza kudaiwa marejesho ya mkopo, jambo lililomlazimu kukopa sehemu nyingine ili kulipa.
Kabla ya Kuuzwa. Baada ya Kuuzwa.
Hata hivyo, amesema licha ya jitihada hizo, benki hiyo iliuza mali zake ikiwemo kituo hicho cha mafuta chenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.5 kwa bei ya Sh milioni 600 pekee, bila kufanyika mnada wa wazi.
“Tarehe 25 Juni 2025 walimuuza sheli yangu kwa mtu anayeitwa Muslim Yusufali Bharwani bila mimi kupewa taarifa yoyote. Makabidhiano yalifanyika tarehe 11 Septemba 2025 kwa kuvunja kufuli za geti, jambo nililolifahamu kupitia taarifa kutoka kwa Mtendaji wa Kata ya Kivule,” alisema Niboye.
Ameongeza kuwa mbali na sheli hiyo, eneo jingine lenye fremu 36, ukumbi unaochukua watu 800 na ukubwa wa mita za mraba 5,052, nalo limeuzwa kwa Mbunge wa Ukonga, Jerry William Silaa, kwa Sh milioni 700, wakati thamani halisi ya eneo hilo inakadiriwa kufikia Sh bilioni 3.5.
“Nilikaribia kulia. Nilitegemea kama mbunge wangu angenitetea kama mwananchi wake, lakini badala yake amekuwa sehemu ya kuniangamiza,” alisema kwa masikitiko.
Niboye alifafanua kuwa jumla ya mali zote zilizouzwa zina thamani ya zaidi ya Sh bilioni 7, huku benki ikidai bado anadaiwa Sh milioni 94. Amesema tayari amefungua kesi katika Mahakama Kuu, lakini bado amekuwa akifukuzwa kwa nguvu kwenye maeneo hayo na wapangaji wake kuondolewa bila taratibu.
Amedai kuwa benki ilipokea fedha za mauzo tarehe 4 na 20 Juni 2025, kabla hata ya kutangaza mnada katika gazeti la Zanzibar Leo la tarehe 18 Juni 2025, lililotangaza mnada huo ungefanyika tarehe 25 Juni 2025.
“Tangazo lile lilikuwa danganya toto. Fedha za mauzo zilishapokelewa kabla hata ya tangazo, huu ni ubabaishaji na unyanyasaji mkubwa kwa wananchi wanaochukua mikopo kwa imani njema,” alisema Niboye.
Kwa sasa, Niboye anaiomba Benki Kuu kufanya uchunguzi wa kina kuhusu utendaji wa Benki ya Equity, na kuomba uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzuia mauzo ya mali zake zilizobaki ikiwemo ukumbi, baa na nyumba za kulala wageni (guest house) zilizopo Viwege, Kata ya Majohe.
“Sijashindwa kulipa. Nina uwezo wa kulipa. Ninachoomba ni haki na kufuatwa kwa taratibu,” alisisitiza.
Mamlaka za Serikali za Mitaa nazo zatia shaka juu ya mauzo hayo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni B, Ali Bakari Kipako, amesema kuwa mnamo Septemba 29, 2025, alipokea notisi nyingi kutoka kwa kampuni ya udalali ya BILO, zikiwaelekeza wapangaji wa fremu za biashara za Moshi Bar kuhama ndani ya siku 14 kwa madai kuwa eneo limeuzwa na benki.
“Nilishangazwa kwa sababu taratibu za kibenki zinajulikana. Mwananchi anapokopa kupitia benki, sisi viongozi wa mtaa tunatoa barua ya utambulisho. Lakini katika mauzo haya hatukupewa taarifa yoyote,” alisema Kipako.
Ameeleza kuwa baada ya kushauriana na Mtendaji wa Kata, ambaye ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, walikubaliana kutokubali notisi hizo kwa kuwa hazikuwa na uhalali.
“Baada ya kukataa kupokea notisi, maafisa wa kampuni hiyo ya udalali walifika tena na kuanza kuwatishia wapangaji wa fremu kwamba waondoke mara moja au walipie kodi mara mbili. Huo ni uhuni na ukiukwaji wa haki,” alisema Kipako.
Ameongeza kuwa tukio hilo limewafanya baadhi ya wananchi kukosa imani na serikali, kiasi cha kugoma kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, wakisema hawajatendewa haki.
Balozi wa Shina namba 8 naye atilia shaka
Kwa upande wake, Balozi wa Shina namba 8 wa Kipunguni B, Pascal Thomas, alieleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa kushiriki kugawa notisi kwa wapangaji wa fremu hizo.
“Niliuliza kinachoendelea nikaambiwa tunagawa notisi za siku 14 kwa wapangaji wa Moshi Bar. Nilitii amri kama ilivyotoka juu,” alisema.
Hata hivyo, amesema bado ana mashaka juu ya uhalali wa mauzo hayo kwa kuwa anamfahamu Mzee Moshi Bar kama mtu mwenye uwezo wa kifedha na siyo mkopaji aliyeshindwa kurejesha.
“Kwa sisi tunaomfahamu Mzee Moshi Bar, kusema ameshindwa kulipa mkopo ni jambo la kututia shaka kubwa,” alisema Balozi huyo.
Wakili Benki haziko juu ya sheria
Wakili wa Paschal Niboye( Mzee Moshi Bar), Benedictor Wagenda, amesema sheria ya mikopo na dhamana (The Mortgage Financing Act) inataka kabla ya mali ya mdaiwa kuuzwa, benki ihakikishe imekamilisha hatua zote za kutoa taarifa rasmi, kuonya, na kutoa muda wa kutosha wa marekebisho.
“Kama kweli mauzo yalifanyika kabla ya tangazo la mnada, ni ukiukaji mkubwa wa kifungu cha 13 cha Sheria ya Mikopo na Dhamana. Benki inapaswa kumjulisha mdaiwa kwa maandishi, kutoa muda wa marekebisho, na kisha kuchapisha tangazo la mnada lenye uwazi,” alisema.
Amesisitiza kuwa wananchi wengi wanaingia kwenye hatari kutokana na ukosefu wa elimu ya mikataba ya mikopo na kutojua haki zao pindi wanapopata matatizo ya marejesho.
“Haki ya kumilikishwa taarifa na kushirikishwa katika mchakato wa mnada ni haki ya kikatiba. Hata kama mdaiwa ana deni, haina maana benki iwe na mamlaka ya kufanya mauzo kwa kificho,” aliongeza.





.jpeg)






