Na Miraji Msala, Mkuranga – Pwani
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kutekeleza miradi mikubwa yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.2, ikilenga kurahisisha usafiri na kuinua uchumi wa wananchi wa vijijini na mijini.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Silas Dilliwa, amesema miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuboresha barabara kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema miongoni mwa miradi inayoendelea ni ujenzi wa barabara ya Vikindu–Sengetini yenye urefu wa kilomita 18.66, inayounganisha Wilaya ya Mkuranga na Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Ubaruku Construction Co. Ltd, ulianza tarehe 20 Agosti 2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 20 Februari 2026, ukiwa umefikia asilimia 60 ya utekelezaji, kwa gharama ya shilingi bilioni 1.351.
“Mradi huu utatatua changamoto za usafiri hasa wakati wa mvua, ambapo awali barabara ilikuwa haipitiki. Kwa sasa tumejikita katika ujenzi wa mifereji yenye urefu wa mita 1,200 na mitaro yenye kina cha mita 1.8 ili kudhibiti maji ya mvua,” alisema Mhandisi Dilliwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Aidan Maliva kutoka Kampuni ya Ubaruku amesema kazi inaendelea kwa kasi na kwa viwango vya juu, huku wakifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Aidha, Meneja Dilliwa alitembelea pia mradi wa ujenzi wa barabara ya zege ya Nyamaronda–Nasibugani yenye urefu wa mita 400, uliogharimu shilingi milioni 531.5 na kukamilika kwa asilimia 100.
Amesema lengo la kuweka zege katika eneo la mlima Lukanga lilikuwa kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote, ambapo ujenzi huo ulifanywa na Kampuni ya Link Construction Company Ltd, ambayo ni ya wazawa.
Vilevile, TARURA Mkuranga imetekeleza ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika mji wa Mkuranga, kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Barabara hizo zenye urefu wa mita 650 ni pamoja na Mkuranga–Dondwe (mita 350), Bomani–Sunguvuni (mita 300) na ukarabati wa barabara za Magawa–Nganje na Magawa–Mdimni, kwa gharama ya shilingi milioni 836.4.
“Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, na lengo kuu lilikuwa kuboresha mwonekano wa mji wa Mkuranga kwa kuweka barabara za lami zinazodumu kwa muda mrefu,” alisema Mhandisi Dilliwa.
Kwa upande wake, mkazi wa Vianzi, Said Tinyago, ameishukuru TARURA na Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi za kuboresha barabara, akisema awali wananchi walilazimika kutumia mianzi kuvuka maeneo yenye tope.
“Kipindi cha mvua tulikuwa tunapata shida kubwa ya usafiri, lakini sasa tunashukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia kwa kutuletea maendeleo haya makubwa,” alisema Tinyago.
Utekelezaji wa miradi hiyo unaifanya Wilaya ya Mkuranga kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza mkoani Pwani kwa kasi ya kuboresha miundombinu ya barabara, hatua inayotarajiwa kuongeza tija katika biashara, kilimo na huduma za kijamii.















