Na Miraji Msala-Rufiji
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Nicolas Ludigery, amesema miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja inayotekelezwa wilayani humo inaendelea vizuri, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu ya usafiri na kuinua shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi minne ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 25, Ludigery alisema ujenzi huo unalenga kuboresha huduma za usafiri, kukuza biashara, na kuongeza fursa za kijamii katika maeneo ya vijijini.
Lengo letu ni kuhakikisha Rufiji inakuwa na miundombinu bora ya barabara itakayochochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na elimu. Tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwa wakati, jambo lililowezesha kazi kwenda vizuri,” alisema Ludigery.
Mradi wa kwanza ni Daraja la Mhoro, lenye urefu wa mita 100 na kilometa moja ya barabara ya lami, unaogharimu shilingi bilioni 17.8. Mradi huo ulianza Januari 31, 2024 na unatarajiwa kukamilika Machi 24, 2026.
Mradi wa pili ni barabara ya Chumbi–Kiengere, yenye urefu wa kilometa 1.2, ambayo imekamilika kwa asilimia 100. Barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami na ina taa za barabarani pamoja na mifereji ya maji ya mvua. Inatarajiwa kurahisisha mawasiliano kati ya Rufiji na Kibiti, na hivyo kuchochea shughuli za uchumi, afya na elimu.
Aidha, barabara ya Ikwiriri yenye urefu wa kilometa 6, inajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 6.3. Mradi huo ulianza Septemba 8, 2025 na unatarajiwa kukamilika Februari 3, 2026, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 20.
Mradi mwingine ni barabara ya Ikwiriri–Myuyu, yenye urefu wa mita 700, inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 999, na hadi sasa imefikia asilimia 80 ya utekelezaji.
Daraja la Mhoro Kubadilisha Maisha
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Daraja la Mhoro, Mhandisi Emanuel Mahimbo, alisema daraja hilo lina urefu wa mita 100 na kina cha mita 8.9, na hadi sasa limefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Awali, mradi huo ulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 11.5, lakini kutokana na mafuriko makubwa yaliyotokea katika eneo hilo, gharama ziliongezeka hadi bilioni 17.8.
Daraja hili likikamilika litaunganisha kata ya Mhoro Magharibi na kata ya Shea, na kurahisisha huduma kama elimu, afya na biashara. Shukrani kwa Serikali kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutupatia fedha kwa wakati na kwa Mbunge wetu Mohamed Mchingelwa kwa ushirikiano mkubwa,” alisema Mahimbo.
Baadhi ya wananchi wa eneo la Mhoro wameeleza furaha yao kutokana na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, wakisema utaleta mabadiliko makubwa katika maisha yao ya kila siku.
Bi Shida Mohamedi, mkazi wa Mhoro, alisema kabla ya kuanza kwa mradi huo kulikuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano hasa wakati wa mvua
Tulikuwa tunavuka kwa shida, watoto walishindwa kwenda shule na wagonjwa walikwama kufika hospitali. Sasa tunashukuru sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea daraja hili. Limekuwa tumaini letu jipya,” alisema kwa furaha.
Kaimu Meneja Ludigery aliwataka wananchi wa Rufiji kutunza miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
Tunaomba wananchi wasitupe taka kwenye mifereji ya maji wala kando ya barabara. Pia tunatarajia kufunga taa za barabarani ili kuongeza usalama na urembo wa mji,” alisema.
Kwa ujumla, zaidi ya kilomita 14 za barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami wilayani Rufiji, hatua inayotarajiwa kubadilisha kabisa sura ya mji wa Ikuriri na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
















