Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kukoboa kahawa cha MCCCO kilichopo wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakiendelea na majukumu yao.

Meneja Masoko wa kiwanda cha kukoboa kahawa cha MCCCO kilichopo wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma David Haule kitoa taarifa ya upokeaji na ukoboaji kahawa katika kiwanda hicho inayoletwa na wakulimu.
……………
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WAKULIMA wa zao la kahawa kutoka Vyama mbalimbali vya msingi vya Ushirika katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuendelee kukiimarisha kiwanda cha kukoboa kahawa cha Mbinga Coffee Curing Company(MCCCO) ili waweze kunufaika na soko la kahawa wanayozalisha.
Wamesema,licha ya nguvu kubwa wanayotumia katika uzalishaji wa zao hilo lakini changamoto kubwa ni sehemu ya kuhifadhi kahawa kwani maghala yaliyopo ni machache ikilinganisha na kahawa inayoletwa kutoka kwenye vyama vyao vya Ushirika.
Oscar Nchimbi amesema,kiwanda hicho kimekuwa mkombozi mkubwa kwani ndiyo sehemu sahihi inayofaa kwa kuhifadhi kahawa,kupata vipimo sahihi na kukoboa kahawa kabla ya kupeleka kwenye minada kwa ajili ya kuuzwa.
Otin Kapinga amesema,kiwanda cha MCCCO ndicho kinachoongoza kwa kuchakata kahawa vizuri tofauti na viwanda vinavyomiliiwa na watu binafsi ambapo amewapongeza wafanyakazi wa kiwanda kwa kutoa huduma nzuri kwa wakulima.
Kapinga amesema,inayosindikwa na kiwanda hicho ni bora hali iliyowezesha wakulima kupata soko zuri na la uhakika wanapofikisha kahawa mnadani kwa ajili ya kuuzwa.
Kwa upande wake Meneja mauzo na masoko wa kiwanda cha MCCCO David Haule amesema,kiwanda hicho kikongwe katika Mkoa wa Ruvuma kilichoanzishwa mwaka 1986 kina uwezo wa kukoboa zaidi ya tani 35,000 kwa mwaka.
Haule amesema,kiwanda cha MCCCO kilikuwa ndiyo kiwanda pekee cha kuchakata kahawa katika mkoa wa Ruvuma, na kilianzishwa kwa lengo kuwaondolea wakulima usumbufu wa kupeleka kahawa katika mikoa mingine hapa nchini kwa ajili ya ukoboaji.
“Tangu kilipoanzishwa hadi sasa licha ya kufunguliwa viwanda vingine vidogo,lakini zaidi ya asilimia 60 ya kahawa inayolimwa katika Wilaya ya Mbinga inaletwa hapa MCCCO kwa ajili ya uchakataji,tuna sababu ya kuchukua nafasi kubwa kutokana na ufanisi wa kiwanda chetu kwani tuna uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 35,000 kwa mwaka japo hatujawahi kufikisha kiasi hicho”alisema Haule.
Ametaja sababu nyingine ni kiwanda hicho kumilikiwa kwa ubia kati ya vyama vya msingi vya ushirika vinavyolima hisa kwa asilimia 56.54 huku Serikali inamiliki asilimia hisa 43.46.
Haule ametaja kazi inayofanyika katika kiwanda hicho ni ukoboaji kahawa ghafi inayotoka kwa vyama vya ushirika,makampuni na watu binafsi,kuhifadhi kahawa safi iliyochakatwa katika ubora wa hali ya juu na utengenezaji wa bidhaa za kahawa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma”amesema.
“Bidhaa zetu zinafahamika kwa jina la Mbinga Coffee,dhamira kubwa ya kiwanda ni kuhamasisha unywaji wa soko la ndani na tunaona katika jitihada zinazofanywa na wazalishaji wa ndani umeongezeka kutoka asilimia 3 ya awali hadi kufikia asilimia 7”amesema Haule.
Aidha amesema,licha ya kuongeza thamani ya zao la kahawa lakini kiwanda hicho kina umuhimu mkubwa kwa Taifa hasa kwa wananchi kupata ajira za kudumu na ajira za msimu ambapo kuna watu zaidi 300 ambao wanafanya kazi mbalimbali sambamba na kulipa kodi kwa Serikali na kutoa gawiwo kila mwaka.
Meneja uzalishaji msaidizi wa mitambo wa kiwanda hicho Mkombozi Sanga amesema,hadi sasa kiasi cha kahawa iliyopokelewa kwa ajili ya kukoboa ni zaidi ya tani 11,000 kutoka kwa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos).
Sanga amesema,kahawa inayopokelewa na katika kiwanda hicho ni safi isiyokuwa na unyevu ili kuwezesha kukoboleka vizuri kwenye mashine.”alisema.









