Na Yohana Kidaga- Ngorongo, Rufiji
Mgombea wa Ubunge jimbo la Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kumchagua tena katika kipindi atahakikisha anaiomba Serikali iweze kukamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mkongo, Ngorongo hadi Ikwiriri kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM ili kuifungua Wilaya ya Rufiji na mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kukiombea kura Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu kwa ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani katika Kijiji cha Kilimani kata ya Ngorongo jimboni Rufiji, ambapo pia aliwapokea wanachama kadhaa kutoka upinzani, Mhe. Mchengerwa amesema pamoja na kwamba tayari CCM kimefanya mambo makubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ambao umehusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na taa za umeme, madaraja makubwa ya kisasa, stendi na masoko lakini bado atahakikisha wananchi wa kata Ngorongo wanajengewa barabara ya kisasa ya kiwango cha lami.
“Ndugu zangu naomba niendelee kuwahakikishia kuwa kama mgombea Urais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi Oktoba 20, kwenye mkutano wake wa kampeni pale Ikwiriri kwamba atahakikisha Serikali inakamilisha kazi nzuri iliyoanza ya ujenzi wa barabara basi mimi kama Mbunge na mtumishi wenu nitahakikisha nasimamia utekelezaji wa ahadi za Mhe. Rais kwa masilahi mapana ya Wanarufiji na watanzania kwa ujumla”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amefafanua kuwa katika kipindi chake alipokea jimbo likiwa hakuna hata nusu kilomita ya barabara ya kiwango cha lami lakini sasa mitaa yote ya Ikwiriri na barabara za kila kona za Wilaya ya Rufiji zimeanza kutengeneza kilichobaki ni kumaliziwa tu.
Kuhusu madai ya kunyang’anywa ardhi ya Kijiji cha Kilimani, Mhe. Mchengerwa amewahakikishia wananchi wa kata ya Ngorongo kuwa hakuna mtu anayeweza kutwaa ardhi ya Kijiji hicho bila taratibu za kisheria na kwamba tayari jambo hilo lilishajadiliwa na vikao vya madiwani na kupatiwa ufumbuzi hivyo hakuna sababu ya kuwa na mashaka kwani tayari limeshafanyiwa kazi.
Aidha, amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Ngorongo kwa kuendelea kukiamini CCM na yeye binafsi kutoa kura nyingi bila kutaka kupewa rushwa ili wakipigie kura.
“Kwa dhati ya moyo wangu ninawashukuru wana Ngorongo kwa heshima mnayoendelea kutoa kwa CCM na kwangu binafsi kwa kupiga kura nyingi kwenye kila uchaguzi kwa kuzingatia kazi kubwa tuliyoifanya ni matumaini yangu pia kwenye uchaguzi huu mtapiga kura nyingi za heshima kwa CCM, ahsante sana”. Ameshukuru Mhe. Mchengerwa
Amewaomba watu kujitokeza siku ya kupiga kura bila hofu yoyote na kuitumia haki yao ya kikatiba kupiga kura kwa amani na kusuburi matokeo majumbani.
Mhe. Mchengerwa anaendelea na mikutano ya hadhara katika kata nyingine za Jimbo hilo kuomba kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa madiwani na kwake mwenyewe ili apewe ridhaa ya kuwaongoza tena katika kipindi hiki.
Mhe. Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia Mhe. Bibi Titi Mohamed ambapo anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.
Licha ya kuwa Mbunge wa tisa wa Jimbo hilo, Mhe. Mchengerwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache nchini ambao wamehudumu kwenye mihimili yote katika nafasi za juu za uandamizi.
Akiwa kwenye mkutano wa kampeni zake alioufanya Ikwiriri, Mgombea wa Urais, mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimwelezea Mhe Mchengerwa kuwa amefanya kazi nzuri katika Wizara zote nne alizomteua kuhudumu kwenye kipindi chake cha uongozi.










