Wito umetolewa kwa vijana ifikapo Oktoba 29, 2025 kujitokeza katika vituo vya kupigia kura na kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kuchagua viongozi kuanzia ngazi ya Urais, Wabunge na Madiwani ambao watashirikiana pamoja katika kuwaletea maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Bi. Jenista Mhagama, Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Peramiho (Ruvuma) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo Oktoba 25, 2025 wakati aliposhiriki kwenye Bonanza la Afya, wilaya ya Songea vIjijini llilofanyika katika uwanja wa Tamasha, Peramiho.
“Tunapoelekea tarehe 29, 2025 bonanza letu limebeba ujumbe maalum, ikiwemo kuhamasisha vijana wote katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kutekeleza wajibu wao wa kikatiba,” amesema Bi. Mhagama.
Amesema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea vijana wapo wengi, hivyo kupitia bonanza hilo amewataka kufikisha ujumbe huo kwa vijana wengi zaidi ili waweze kutambua umuhimu wa zoezi lililo mbele yao.
“Tumekumbushana kuwa katika Jimbo la Peramiho sisi ni watu wa amani, tumezoea kuwa na amani na tunatamani kuwa ni chachu ya amani katika maeneo mengine yote,” amesisitiza Bi. Mhagama na kuwataka vijana kuwa mabalozi wa amani na kutoa taarifa yeyote ya viashiria vya uvunjivu wa amani.
Bi.Mhagama amewataka wananchi kupitia imani zao kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili Taifa liendelee kuwa na amani na kuvuka salama katika kipindi hiki cha uchaguzi na kupata Viongozi bora watakao waletea maendeleo wananchi.









