Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdallah Ulega, leo amefunga rasmi kampeni zake za ubunge na kuwaomba wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
“Asiyeshukuru kwa yai, hata jogoo hachinjiwi. Nendeni mkamchague Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkanichague mimi kijana wenu, pamoja na madiwani wetu wa kata zote za Jimbo la Mkuranga,” alisema Ulega.
Ulega alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Wilaya ya Mkuranga imepata miradi mikubwa ya maendeleo kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji na barabara.
Aidha, Mgombea huyo wa CCM alitumia mkutano huo kuwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha uchaguzi mkuu utafanyika kwa amani, utulivu na haki, bila mwananchi yeyote kudhurika.
“Serikali haiwezi kuruhusu haki ya wananchi kupiga kura ivurugwe na watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza taharuki. Tumewekeza kwa kiwango kikubwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia unaimarishwa,” aliongeza Ulega.









