

Dodoma, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokelewa kwa shangwe na watumishi wa Ofisi ya Rais, Ikulu, alipowasili katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa rasmi kuendelea na majukumu yake ya kuliongoza taifa.
Mhe. Rais Samia aliwasili katika Ikulu hiyo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa serikali, ambapo alipokelewa kwa heshima kubwa ikiwemo nyimbo za kizalendo na vifijo kutoka kwa watumishi wa Ofisi ya Rais waliokuwa na furaha kumuona kiongozi wao mkuu.
Mara baada ya mapokezi, Mhe. Rais alikutana na watumishi wa Ofisi ya Rais na kuwashukuru kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma katika kulitumikia taifa. Aidha, aliwahimiza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.








