NA DENIS MLOWE, IRINGA
DIWANI wa Kata ya Mshindo,, Ibrahim Ngwada amechaguliwa kwa kishindo kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kuendelea kuwa meya kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Ngwada amechaguliwa kwa kura zote 25 za ndio akiwa mgombea pekee katika uchaguzi huo uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Manispaa hiyo mkoani Iringa.
Akitangaza kura zilizopigwa kwa ajili ya Meya na Naibu Meya, Mwenyekiti wa Uchaguzi huo Katibu tawala wa wilaya ya Iringa, Benard Urasa alisema kuwa madiwani waliiopiga kura walikuwa 25 ambapo wote walimpa kura za ndio akiwemo mbunge wa Iringa mjini, Fadhil Ngajilo aliyekamilisha idadi ya madiwani 25.
Naye Diwani wa kata ya Nduli, Bashiri Mtove amechakuliwa kuwa Naibu Meya wa manispaa kwa kura 24 za ndio huku kura moja ikisema hapana ambapo atahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Ngwada amewashukuru madiwani wenzake na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano katika kipindi alichopewa na kufikia malengo waliyokusudia.
“Naikishukuru chama changu (Chama Cha Mapinduzi-CCM), ambacho ndicho kilimelipitisha jina lake kuwa miongoni mwa wagombea na kisha kupigiwa kura kuwa Meya kwa mara nyingine.”Alisema
Aidha aliwashukuru madiwani kwa kumpa kura za kishindo kuwa Meya na kuwaongoza tena kwa miaka 5 na kuahidi kuwa litakuwa baraza lenye kuwasikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto ambazo atahakikisha zinatatuliwa ni hali ya miundombinu ya barabara katika kata zote za Iringa mjini.







