Jeshi la Polisi Tanzania linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha ya watu na mali zao sambamba na kuhakikisha hali ya amani, utulivu na usalama unaendelea kuimarika nchini.
Pia, limeendelea kuzuia uhalifu sambamba na kuwakamata wale wanaofanya makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya kimtandao kama yale ya wanao endesha makundi mbalimbali katika mitandao ya kijamii ya kuhamasisha uhalifu na kuwachulia hatua kama sheria za nchi zinavyoelekeza.
Aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikifuatilia kwa karibu sana yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na kwenye makundi sogozi wakihamasisha wanayo yaita maandamano ya amani yasiyo na kikomo tarehe 9 Disemba 2025.
Hicho wanachohamasisha na kukiita maandamano ya amani mtu yeyote aliyewasikiliza na akaendelea kuwasikiliza wanahamasishana kufanya mambo yafuatayo;
1. Siku hiyo ya maandamano yasiyo na kikomo yaani tarehe 9 Disemba 2025 wanaelekezana ambaye hajui kutumia silaha na hajapitia mafunzo siku hiyo asishike silaha wawaachie waliopata mafunzo ya matumizi ya silaha.(Kwa maana rahisi watu hawa wanazo silaha za kutimiza lengo ambalo wamekusudia).
2. Kupitia mitandao na klabu mbalimbali za mtandaoni wanahamasishana ili kusiwe na shughuli yoyote itakayokuwa inaendelea.
3. Pia wahakikishe wanaharibu na kuchoma moto minara yote ya mawasiliano ili nchi nzima ikose mawasiliano.
4. Wanahamasishana wahakikishe bandari ya Dar es Salaam haifanyi kazi kwani watafunga barabara zote za kuingia na kutoka bandarini.
5. Siku hiyo na kuendelea wanahamasishana wafunge barabara zote za kuingia na kutoka katika mipaka yote ili kuhakikisha hakuna anayetoka au kuingia nchini.
6. Wanahamasishana kama vijana wakapore mali za watu kwasababu wanacho kisingizio kuwa wana njaa.
7. Uhamasishaji huo umekwenda mbali zaidi kwa kuhamasisha siku hiyo waende pia kwenye mahospitali ili kuzuia huduma kwa wagonjwa zisitolewe kwani wakifanya hivyo nchi itasimama.
8. Pia wanahamasishana kuwa, watahakikisha wanawafuata popote walipo watumishi wa serikali ili wawadhuru.
9. Wakati hayo yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii tumesikia matamko mbalimbali na wanao yatoa wanasema, wanaohamasisha na wanaohamasishwa wakiandamana siku hiyo tutawakuta wamekatana vichwa huko mitaani.
10. Wapo wengine wameapa na kutamka watakaoandamana wasifike kwenye Mitaa yao kwani watawashughulikia ipasavyo.
11. Wengine wanasema hawatakubali tena kupata hasara waliyoipata tarehe 29.10.2025 na siku zilizofuata hivyo watahakikisha tarehe 9.12.2025 na kuendelea wanalinda maisha yao, familia zao na mali zao ili asitokee mtu wa kuwazuia kuendelea na shughuli zao.
12. Wengine wanauliza wanaohamasisha maandamano yasiyo na kikomo ni haki ya aina gani hiyo? Kwasababu huwezi kujitangazia haki ambayo inavunja haki za wengine kwa kuwazuia wasiendelee na shughuli zao hasa zinazowapatia riziki ya kila siku, kwani mtu anapotoka na akajishughulisha katika shughuli halali ndiyo mkono unaingia kinywani. Ukinizuia kutoka unavunja haki zangu na unataka kuniua mimi kwa njaa pamoja na familia yangu au wategemezi wangu.
Maandamano ya siyo na kikomo maana yake unataka bidhaa zisifike kwenye masoko halafu tule nini?
Hayo ndiyo yanayoendelea na yanayo hamasishwa kupitia Mitandao ya Kijamii na kwa njia zingine na yanasikika kila siku na kila mtu na yanaleta hofu kwa Jamii.
Huu ni uhalifu mkubwa unaoendelea kuhamasishwa. Hali kama hii kwa nchi yeyote ile dunia ni tishio kubwa la maisha ya watu, uchumi wa nchi na masuala yote ya Kijamii.
Hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zao kuanzia ngazi za familia wawakatae watu kama hawa pamoja na wanayoyahamasisha kwani malengo yao ni kuharibu taifa letu na kuturudisha kwenye machungu na madhara tuliyoyapata tarehe 29/10/2025 na siku zilizofuata.
Taifa letu linahitaji uponyaji kama jitihada za Viongozi wetu wa kitaifa zinavyoendelea kufanyika hivi sasa na hatuhitaji tena vurugu.
Aidha, mwezi huu wa Disemba tunaelekea kwenye maandalizi ya sherehe za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka. Jeshi la Polisi linawahimiza wananchi kuendelea na maandalizi mazuri yanayozingatia usalama wa maisha na mali zao. Watakao safiri wahakikishe wanaacha waangalizi au walinzi katika makazi yao. Vile vile wazingatie sheria za usalama barabarani na kufuata ishara mbalimbali zilizopo katika barabara zetu ili kuepuka ajali.
Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi wote wapenda amani kuwa, litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kulinda maslahi ya taifa, maisha ya watu na mali zao na vitahakikisha amani, utulivu na usalama unaendelea kuimarika nchini.
Imetolewa na;
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma,Tanzania





