Na Meleka Kulwa-Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa imesogeza huduma zake za afya hadi katika Viwanja vya Mnadani Msalato jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto ambayo huadhimishwa duniani kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka. Hatua hiyo imelenga kuwafikia wananchi ambao mara nyingi hawafiki hospitalini kupata huduma za kiafya au elimu kuhusu ukatili.
Maadhimisho hayo yamefanyika Desemba 6, 2025, na kilele chake kitakuwa Desemba 10, 2025.
B. Hindu Ibrahim, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Ubunifu wa hospitali hiyo na Mratibu wa Huduma za masuala ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, amesema kuwa timu ya madaktari, wanasheria na wataalamu mbalimbali imefika Msalato Mnadani ili kutoa huduma hizo moja kwa moja kwa wananchi. Aidha, amesema kuwa hawakutaka kuja kwa ajili ya kutoa elimu pekee, bali pia kutoa huduma za vitendo ikiwemo kupima afya, uchangiaji damu na huduma za afya ya akili.
Katika kambi hiyo, wananchi wamepima uzito, presha na vipimo vingine vya awali, huku wale waliotaka kuchangia damu wakifanya hivyo papo hapo. Aidha, amebainisha kuwa vipimo vingine vitakavyofanyika vitatolewa majibu bure baada ya siku chache.
Aidha, Bi. Hindu amesema kuwa Msalato Mnadani ni eneo linalokusanya watu wengi wanaokuja kwa shughuli zao za kawaida, na mara nyingi hawapati muda wa kufika hospitalini au kufikiwa na elimu ya afya. Aidha, amesema kuwa kusogeza huduma katika eneo hilo kumewawezesha kuwafikia watu ambao huenda hawajapima afya kwa muda mrefu, hivyo kuwapa nafasi ya kupata huduma hizo karibu na walipo.
Aidha, ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi kuchangia damu, huku akibainisha kuwa, “Huduma hizi ni bure na hata akija Benjamin Mkapa. Kuna baadhi ya huduma pia zitakuwa bure, lakini baadhi zitachangia kulingana na shida yake,” amesema Bi. Hindu.
Baadhi ya wananchi waliofika kutembelea banda hilo, Ratifa Abdalah, mkazi wa Miyuji, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa sababu husaidia kuokoa maisha ya watu wanaohitaji damu kutokana na ajali au magonjwa. Aidha, amesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma bora na nzuri.
Kwa upande wake, Sauda Omary, mkazi wa Msalato, amesema kuwa wananchi wanapaswa kujitokeza kupima na kujua afya zao, akibainisha kuwa huduma zilizofikishwa Msalato zimekuwa msaada mkubwa kwa sababu zimewasogelea wananchi ambao hupata changamoto ya kufika hospitalini. Aidha, ameishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kusogeza huduma hizo karibu na jamii.








