Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Zuber Lihuwi,akitoa salamu za Chama hicho kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani,kulia Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo Fransis Mgoloka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Philemon Magesa,akizungumza kwenye kikao hicho.
…………
Na Mwandishi maalum, Namtumbo
CHAMA cha Mapinduzi(CCM)Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma,kimewaonya madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo,kuepuka kuwa chanzo cha migogoro na majungu baina yao kwani migogoro ni sumu mbaya inayoweza kukwamisha juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaleta maendeleo wananchi wa Wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Zuber Lihuwi,wakati akitoa salamu za Chama hicho kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la madiwani kilichohudhuriwa na baadhi ya watumishi,wakuu wa idara na vitengo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mjini Namtumbo.
Alisema,ushirikiano kati madiwani na watumishi ni kitu muhimu na ugomvi kati ya pande hizo mbili ni sumu kwa maendeleo ya Halmashauri kwa kuwa watakaohumia ni wananchi wa kawaida kwa kukosa huduma muhimu za kijamii.
“Niwaombe sana waheshimiwa madiwani,twendeni tukafanye kazi kwa ushirikiano,majungu na mifarakano ni adui mkubwa wa maendeleo tuachane nayo kabisa,nyinyi madiwani na watumishi ni wamoja na mkishirikiana mnaweza kuipeleka Wilaya yetu mbali sana kimaendeleo”alisema Lihuwi.
Amewakumbusha madiwani hao,kuepuka kuwa Miungu watu badala yake kwenda kuwatumikia wananchi kwa uadilifu,uaminifu,heshima na kusimami vyema miradi itakayotekelezwa katika kata zao ili ileta tija inayokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Philemon Magesa alisema,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri imetekeleza jumla ya miradi 110 yenye thamani ya Sh.5,564,069,581.37 ikiwa miradi 51 iliyovuka mwaka wa fedha 2023/2024 na miradi iliyopokea fedha kwa mwaka 2024/2025 ni 59.
Magesa alisema,hadi kufikia Juni 30 mwaka 2025 jumla ya miradi 101 kati ya 110 ilikuwa imekamilika kwa asilimia 100 na miradi 9 ikiwa kwenye ukamilishaji kwa asilimia 98 ambapo jumla ya Sh.5,420,998,887.35 zilikuwa zimetumika saw ana asilimia 97.4 ya fedha zote ambazo zilipokelewa.
Aidha Magesa alisema,mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo 104 yenye thamani ya Sh.4,603,088,505.58 na miradi iliyovuka mwaka wa fedha 2024/2025 ni 28 na miradi 5 kati ya 104 ilikuwa imekamilika kwa asilimia 100 na miradi 99 ipo kwenye hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Alisema,katika kutekeleza miradi hiyo jumla ya Sh.1,781,107,533.15 sawa na asilimia 39 ya fedha yote iliyopokelewa kwa mwaka wa fedha hadi kufikia mwezi Novemba 2025.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo Fransis Mgoloka,amewataka madiwani kwenda kufanya kazi kwa bidii, kutimiza ahadi walizotoa kwa wapiga kura wao wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Amewasisitiza madiwani,kuhakikisha wana kwenda kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutatua kero za wananchi kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuibua vyanzo vipya vya mapato kwenye maeneo yao badala ya kazi hiyo kufanywa na watendaji wa Serikali peke yao.
“madiwani ni viongozi na ndiyo wenyeviti wa kamati za maendeleo za kata,hivyo mna wajibu mkubwa kuhakikisha mnashirikiana na watendaji kwa kuibua na kutafuta vyanzo vipya ambavyo ni muhimu sana katika Halmashauri yenu badala ya kutegemea vyanzo mlivyovikuta”alisema Mngoloka.
Baadhi ya wananchi wa Namtumbo,wamewaomba viongozi hususani wanasiasa kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuwaletea maendeleo wanayosubiri kwa muda mrefu.
Ali Ngonyani mkazi wa mtaa minazini alisema,kwenye majungu hakuna maendeleo kwa sababu muda mwingi unatumika kwenye majungu na kuacha kuwatumikia wananchi ambao wanateseka kwa kukosa huduma bora za kijamii ikiwemo maji.
Amempongeza Mwenyekiti wa CCM Wilaya Zuber Lihuwi,kwa kutambua jambo hilo mapema na kulikemea ambapo,ameuomba uongozi wa Chama hicho kuwachukulia hatua viongozi watakaoonekana chanzo cha migogoro na kukosa maelewano kati ya madiwani na watumishi.
Said Aman alisema,mud awa siasa umepita na kilichopo kwa sasa ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na viongozi waliopo madarakani na wao kama wananchi hawapaswi kuwa kikwazo cha utekelezaji wa ahadi hizo.






