*Mkuu wa Gereza Bukoba asema sasa Wafungwa hawaendi nje kutafuta nishati zisizo salama
*Nguvu kazi sasa inaelekezwa katika uzalishaji
*Mkurugenzi Nishati Safi ya Kupikia awapongeza: Ahamasisha ubunifu zaidi
Bukoba
Mkuu wa Gereza la Bukoba, Bw. Aloyce Kalihamwe amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameleta mageuzi makubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Magereza nchini yakichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kazi, kulinda afya na mazingira pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati waliotembelea Gereza la Bukoba kufuatilia utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100, Bw. Kalihamwe amesema nishati safi ya kupikia imeondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili taasisi hiyo hapo awali.
“NIishati safi ya kupikia pamoja na kulinda afya na mazingira, imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wafungwa hawaendi nje ya maeneo ya Gereza kutafuta nishati zisizo salama kama vile kuni, hali iliyokuwa ikihitaji ulinzi mkubwa na rasilimali nyingi.” Amesema
Ameongeza muda ambao ulikuwa ukitumika kwenda nje kulinda wafungwa kwa ajili ya utafutaji wa nishati isiyo safi ya kupikia pamoja na jitihada zilizokuwa zikitumika kuongeza ulinzi sasa zitatumika kufanya mambo mengine ya uzalishaji ndani ya Magereza.
Aidha ametanabaisha kuwa, matumizi ya nishati safi ya kupikia yamepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ununuzi wa kuni pamoja na changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika mchakato wa kuomba vibali vya ukataji miti kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza kikamilifu agizo la Serikali la taasisi zote zinazolisha watu zaidi ya 100 kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Bw. Mlay amesema lengo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha afya na mazingira ya Watanzania yanaimarika kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa hatua iliyochukuliwa na Jeshi la Magereza ni chachu ya kufikia lengo la Serikali la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, Bw. Mlay amelishauri Jeshi la Magereza kuwa na zaidi ya chanzo kimoja cha nishati safi ya kupikia ili kuongeza ufanisi na uhakika wa matumizi ya nishati hiyo, sambamba na kuliasa Jeshi hilo kuendelea kuwa mfano na darasa kwa taasisi nyingine zinazolisha watu zaidi ya 100 nchini, ili zijifunze na kuhamasika kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ilivyofanywa na Magereza yote 129 nchini.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia ameahidi kulipatia Gereza la Bukoba majiko matatu ya kisasa yanayotumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya kisasa na rafiki kwa mazingira katika taasisi za umma.








