Dar es Salaam, Tanzania, 17 Disemba 2025: Pale Tanzania inavyoingia katika msimu wa sikukuu, ambapo safari huongezeka na sherehe kudumu hadi usiku wa manane, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na Bolt wametangaza ushirikiano maalum unaolenga kuwahamasisha Watanzania kufanya maamuzi sahihi na salama, baada ya kusherehekea na kupunguza ajali zinazotokana na kuendesha gari ukiwa umelewa.
Ushirikiano huu, uliozinduliwa jijini Dar es Salaam, unaunganisha kampeni ya unywaji wa kuwajibika ya SBL inayojulikana kama Wrong Side of the Road (WSOTR) na huduma za usafiri za Bolt, ili kufanya usafiri salama kuwa rahisi kupatikana katika kipindi chenye msongamano mkubwa wa magari barabarani. Mpango huu utaendeshwa katika kipindi chote cha sikukuu na unalenga kuhakikisha Watanzania wanafurahia sherehe zao huku wakirudi nyumbani salama.
Kwa kawaida, mwezi wa Disemba huwa ni miongoni mwa miezi ambayo inakua na shughuli nyingi za barabarani nchini, kutokana na safari nyingi, mikusanyiko ya kijamii na matumizi ya pombe. Mchanganyiko huu mara nyingi husababisha kuongezeka kwa ajali za barabarani zinazohusishwa na ulevi. Kupitia ushirikiano huu, SBL na Bolt wanalenga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuhimiza tabia za unywaji salama urahisi na motisha.
Ushirikiano huu ni sehemu ya kampeni endelevu ya Wrong Side of the Road ya SBL, iliyoanzishwa mwaka 2023 chini ya kampeni ya Inawezekana, kuboreshwa mwaka 2024 kama Inawezekana kuwa mtu makini, na kuendelea mwaka 2025 chini ya kaulimbiu Inawezekana Kabisa, Sherehe Salama, Nyumbani Salama. Kampeni hii inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazohusiana na unywaji wa pombe na kuhimiza maamuzi sahihi, hasa katika msimu wa sikukuu.
Kupitia mpango huu, wananchi watakaotazama video ya elimu ya Wrong Side of the Road na kupata cheti chao watapokea Sherehe Code, itakayowapatia punguzo la asilimia 30 kwa safari za Bolt katika kipindi chote cha sikukuu. Aidha, kila safari itampa mtumiaji nafasi ya kuchaguliwa kwa bahati nasibu na kupanda Special Bolt, gari maalum lenye muonekano wa kipekee wa sikukuu, linalotoa uzoefu wa kipekee huku likizingatia usalama.
Kwa kuwahamasisha watu kuacha magari yao na kuchagua usafiri wa kuaminika baada ya kunywa, kampeni hii inalenga kupunguza moja ya hatari kubwa zinazojitokeza wakati wa sikukuu na kuondoa vikwazo vinavyosababisha maamuzi yasiyo salama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya SBL kwa jamii inazozihudumia.
“Disemba ni kipindi kikubwa cha sherehe kwa Watanzania, na kama SBL tunajivunia kuwa sehemu ya furaha hizo. Hata hivyo, hakuna sherehe inayopaswa kuishia katika majonzi. Kupitia ushirikiano huu na Bolt, tunawahimiza watu kufurahia na kuwajibikaji na kufanya maamuzi salama na sahihi ya namna ya kurudi nyumbani,” alisema Hatibu.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Bolt kwa Tanzania, Kenya na Uganda, Dimmy Kanyankole, alisema ushirikiano huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa usafiri salama katika kipindi chenye msongamano mkubwa wa safari.
“Msimu wa sikukuu ni miongoni mwa vipindi vyenye shughuli nyingi zaidi, watu husafiri zaidi, hukaa nje kwa muda mrefu na kufanya maamuzi ya ghafla. Lengo letu ni kuondoa vikwazo vya usafiri salama kwa kuufanya uwe rahisi, nafuu na unaopatikana pale unapohitajika zaidi,” alisema Kanyankole.
Kampeni hii itaendeshwa katika kipindi chote cha sikukuu, ikianza na shughuli katika maeneo makubwa ya burudani na maisha ya usiku jijini Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa kwenda mikoa mingine nchini.
SBL na Bolt wamesisitiza kuwa ujumbe wa kampeni hii ni rahisi: Watanzania hawalazimiki kuchagua kati ya kusherehekea na kurudi nyumbani salama. Inawezekana Kabisa kufanya yote mawili.







