TAARIFA KWA UMMA
Leo ni takriban siku ya 10 toka Jeshi la Polisi Tanzania lilipotoa taarifa ya hali ya usalama nchini tarehe 12/12/2025.
Tungependa kuwajulisha kuwa, kwa kipindi chote hicho hali ya usalama nchini ni shwari pamoja na kwamba kulijitokeza kwa baadhi ya matukio machache ambayo yalishughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.
Ushwari huo umetokana na uelewa wetu kama Watanzania wa umuhimu wa kila mmoja wetu kulinda na kuimarisha amani, utulivu na usalama kwani ndizo nyenzo kuu na za msingi za kumwezesha kila mmoja wetu kushiriki na kufanya shughuli halali zinazotupatia mahitaji yetu ya kila siku.
Tunapoelekea kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka, ambazo zitatanguliwa na sherehe za Krismas, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote na hata baada ya sikukuu hizo.
Aidha, wito unatolewa kwa wananchi wote na kwa wote watakao kuwa nchini kuwa, kinacho hitajika ni kila mmoja wetu kutambua thamani na umuhimu wa amani na usalama katika maisha ya kila mmoja wetu. Pia ni wakati mwafaka wa kuendelea kuyakataa yale ambayo yana malengo ya kuvuruga amani kipindi hiki cha sikukuu na baada.
Maisha yetu na shughuli zetu wakati wa hizi sikukuu yanahitaji mazingira ya amani ili kila mmoja aweze kushiriki kwenye ibada za kumshukuru Mungu, kukaa na familia na marafiki bila bughudha yeyote ile hivyo tuilinde amani kwa ushirikiano na kwa nguvu zetu zote.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wale watakao safiri waendelee kuzingatia Sheria za Usalama barabarani ili zitusaidie kujiepusha na ajali tukizingatia kauli mbinu ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani inayosema “Endesha Salama Familia inakusubiri”.







