Na Neema Mtuka , Sumbawanga
Rukwa:Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha kitengo maalumu cha saa 24 kitakachosikiliza maoni, mapendekezo na kero za wananchi, hususan kutoka makundi maalumu, kwa lengo la kuimarisha ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, wakati wa kikao cha wadau wa mahusiano kilichofanyika leo Desemba 23, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Sangu amesema kitengo hicho kitarahisisha wananchi kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja bila vikwazo vya kiurasimu na kusaidia Serikali kupata mrejesho wa haraka kwa ajili ya kuboresha sera na huduma.
“Kitengo hiki kitafanya kazi saa 24 kwa kuzingatia utu, haki na usawa” amesema Waziri Sangu
Ameeleza kuwa kikao hicho kililenga kutambulisha majukumu ya Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, ikiwemo kuratibu mahusiano ya kisiasa na kijamii kwa kauli mbiu “Mahusiano Imara, Msingi wa Mshikamano wa Kitaifa.”
Akizungumzia ajira kwa vijana, Sangu amesema Makamishna wa Kazi wanapaswa kuhakikisha taarifa za fursa za ajira zinawafikia wananchi kwa wakati.
Amebainisha kuwa mwaka 2025, vijana 5,118 ambapo wanaume walikuwa 3762 na wanawake 1256 walipata ajira za staha nje ya nchi kupitia Wizara yake.
Kuhusu Sekta Binafsi, Sangu amesema kuanzia mwisho wa Januari 2026, kima cha chini cha mshahara kitaongezeka kwa asilimia 33.4, kutoka shilingi 275,060 hadi 358,322, akisisitiza kuwa utekelezaji wake ni wa kisheria na hatua zitachukuliwa kwa waajiri watakaokiuka.
Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa wa Rukwa kushirikiana na Madiwani kuhakikisha fursa za ajira Serikalini na Sekta Binafsi zinawafikia wananchi kwa uwazi na usawa.
Kikao hicho kimesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya uwajibikaji kati ya Serikali na wananchi kwa ajili ya kuimarisha imani, mshikamano wa kitaifa na maendeleo jumuishi.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho akiwemo Lazaro Silas kutoka Chanji ambaye ni bodaboda amesema watumishi wa umma wanapaswa kuwashirikisha vijana fursa mbalimbali zinazojitokeza kwenye maeneo yao ili wanufaike na fursa hizo.
” Vijana hatupati fursa zinawafikiwa wachache ambao wanandugu kwenye ngazi fulani tuliopo chini hatupati taarifa sahihi na hata tukijua tunakuwa tumechelewa ” amesema Silas.









