NA DENIS MLOWE, IRINGA
Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, ametoa wito mkali kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Soko la Kihesa, akimtaka kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa ujenzi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi mbalimbali ndani ya manispaa, Meya Ngwada alisema kuwa kumekuwa na kasumba ya ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali nje ya mkataba hivyo amesema ametembelea na kuzungumza kwa upole wakati huu ila endapo kutakuwa na dalili za kutoridhishwa na kasi ya ujenzi atakuwa mkali zaidi.
Alisema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kurudi katika eneo hilo pindi mradi unapokamilika hivyo kitendo cha ucheleweshaji huo umekuwa ukiwaathiri wafanyabiashara na wananchi ambao wanasubiri kupata soko la kisasa lenye miundombinu bora.
“Tunakumbushana tu tunataka soko hili likamilike kwa wakati. Wananchi wamechoka kusubiri. Hatutakubali tena visingizio vinavyochelewesha maendeleo. Mkandarasi ahakikishe anafanyakazi kwa mujibu wa mkataba,” alisema Meya Ngwada.
Katika ziara hiyo Meya Ngwada aliambatana na madiwani mbalimbali akiwepo naibu meya Bazil Mtove, diwani mwenyeji kata ya Kihesa Hosea Kabelege na diwani wa viti maalum kanda ya hiyo. , Sara Ponela na wataalam wa Manispaa ya Iringa.
Meya Ngwada ameiagiza timu ya usimamizi wa miradi kutoa taarifa za maendeleo mara kwa mara ili kuweka uwazi na kuhakikisha hatua zozote za marekebisho zinachukuliwa mapema na kumtaka afisa maendeleo wa kata kutembelea pia mradi huo wakati wowote kujiridhisha.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa, Bi Sara Ponela alisema kuwa mradi huo muhimu kwa wakazi Kihesa na manispaa kwa ujumla kwani utaongeza mapato ya halmashauri.
Alisema kuwa mradi huo utawasaidia kina mama katika kujiari na kujiongezea kipato hivyo kukamlika kwa wakati utaongeza chachu ya maendeleo na kuipendezesha zaidi manispaa.
Naye Injinia wa Manispaa, Rajabu Msangi alitoa ufafanuzi kuhusu gharama za mradi huo ambapo alisema kuwa jumla ya bilioni 20 zitatumika katika ujenzi wa mradi huo na barabara inayounganisha kata ya Mkimbizi na Mtwivila.
“Tumeweka mkazo zaidi kwenye usimamizi wa karibu ili kuhakikisha kazi inasonga mbele kwa mwendo unaotakiwa. Tutanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha soko linakamilika kama ilivyopangwa.” alisema
Amesisitiza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ujenzi, na kwamba wananchi watarajie soko la kisasa, salama na rafiki kwa wafanyabiashara, mara tu litakapokamilika.
Soko la Kihesa linatarajiwa kuwa moja ya masoko ya mfano katika Manispaa ya Iringa, likiwa na maeneo yaliyopangwa vyema kwa wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali, sehemu za kuhifadhia bidhaa, usafi wa kutosha na miundombinu ya kisasa.








