Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja aliyevaa kaunda suti,akizundua mradi wa malori ya Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu ambayo yamenunuliwa kwa ajili ya kubeba mazao ya wakulima na watu binafsi kama chanzo mojawapo cha mapato ya Chama hicho.(Picha na Muhidin Amri).
Malori mawili kati ya matano yaliyonunuliwa a Chama Kikuu cha Ushirika cha Tamcu Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma a,mbayo yatawezesha kurahisisha ukusanyaji wa mazao ya wakulima kutoka shambani kupeleka kwenye maghala ya vyama vya msingi na Chama Kikuu yakiwa kwenye viwanja vya Chama hicho(Picha na Muhidin Amri).
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tamcu cha Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Denis Masanja(hayupo pichani,wakati wa uzinduzi wa mradi wa malori ya Chama hicho jana uliofanyika katika viwanja vya Tamcu Tunduru mjini(Picha na Muhidin Amri).
……….
Chama Kikuu cha Ushirika Wilayani Tunduru TAMCU,kimenunua jumla ya malori matano kwa gharama ya Sh.1,050,000,000 ambayo yatatumika kubeba mazao ya vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),bidhaa mbalimbali,kukodisha kwa watu binafsi na na makampuni ili kuongeza mapato ya Chama hicho.
Akizundua malori hayo aina ya Howo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja,ameipongeza Bodi ya Chama hicho kwa kutimiza vyema lengo la kununua magari hayo ambayo ni chanzo mojawapo cha mapato.
“Hii ni hatua kubwa kwani Tamcu kupitia Kampuni tanzu ya Tamcu Kampani imeonyesha kwa vitendo uwezo wa kufanya mambo makubwa ya maendeleo ambayo yatakwenda kusaidia chama kuanzisha hata miradi mingi zaidi”alisema Masanja.
Masanja,amewaasa viongozi wa Chama hicho kuhakikisha magari hayo yanatunzwa na kutumika kusafirisha mazao ya wakulima kutoka kwenye vyama vya msingi na kupeleka sokoni badala ya kuyatumia kwa matumizi mengine nje ya malengo yake.
Masanja ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya ya Tunduru,amewataka madereva watakaoajiriwa kufuata na kuzingatia sheria za usalama barabarani na itakuwa aibu kubwa kama magari hayo yatatumika kubeba bangi,mali za wizi,magendo na wahamamiaji haramu.
Masanja,amevitaka vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),kuhakikisha vinanunua magari kwa ajili ya kusafirisha mazao ya wanachama badala ya kukodi magari ya watu binafsi kwa gharama kubwa.
Mwenyekiti wa Tamcu Musa Manjaule alisema,magari mawili yamewasili Wilayani Tunduru na matatu yatawasili mwezi ujao kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu zinazotakiwa kabla ya kuanza kazi.
Alisema,kupitia bodi mpya Tamcu itaendelea kufanya kazi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawezesha kuimarisha shughuli za Chama na wanachama wa Chama hicho na kupitia malori hayo vyama vitafanya shughuli zake kwa uhakika ikilinganishwa na siku za nyuma.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,kuna baadhi ya watu walikuwa wanazungumza maneno ya kukatisha tamaa,lakini kupitia bodi tutaendelea kusimama imara kwa ajili ya wakulima wetu kwa kusimamia mazao ambayo yatauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kama Serikali ilivyoagiza”alisema Manjaule.
Kwa mujibu wa Manjaule,malori hayo yataendeshwa na madereva wa Wilaya ya Tunduru kama sehemu ya kuisaidia Serikali katika kupunguza tatizo kubwa la ajira hususani kwa kundi kubwa la vijana.
Awali meneja Mkuu wa Tamcu Marcelino Mrope,ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kuwatia moyo kwenye utendaji wa majukumu yao ya kila siku licha ya changamoto wanazokutananazo.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa Tamcu Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Namtiti Amcos Mohamed Kalisinje,ameipongeza bodi ya Tamcu Ltd kwa uamuzi wa kununua malori hayo badala ya kutumia magari ya makampuni kwa gharama kubwa.







