Na John Bukuku, Dar es Salaam
Dar es Salaam, 28 Desemba 2025 — Huduma za usafiri kupitia Reli ya Kisasa (SGR) zimeathirika kufuatia hitilafu za umeme zilizosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imethibitisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA, mvua hizo zilizoambatana na upepo mkali kuanzia usiku wa kuamkia leo zimesababisha hitilafu katika mfumo wa umeme wa SGR pamoja na umeme wa TANESCO, hali iliyoathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.
Hata hivyo mmoja wa abiria Bw. Anacleto Pereira abiria ambaye amesafiri na SGR leo kuelekea Dodoma amesema tatizo hilo imeshatatuliwa
na treni zimeanza safari kwa kuchelewa, abiria wa treni ya saa 12:00 asubuhi waliondoka saa 7:40 mchana na wa saa 2: 00 waliondoka saa 8:45 mchana na hivi salsa wako njiani wakiendelea na safari.
Kwa sasa, treni iliyoondoka Dar es Salaam saa 8:45 mchana imefika Ruvu, ambako imesimama kusubiri kupishana na treni inayotoka Dodoma wakati wowote itaendelea na safari.
TMA imeeleza kuwa kuanzia tarehe 26 hadi 29 Desemba 2025, mamlaka hiyo imekuwa ikitoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa katika mikoa mingi nchini, ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Kigoma, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Pwani pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.
Athari za mvua hizo zimeenea pia kwenye miundombinu ya reli ya zamani ya MGR, ambapo madajara yameripotiwa kuathiriwa katika eneo la Kidete wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, na Gulwe wilayani Dodoma, hali inayoongeza changamoto katika sekta ya usafiri wa reli.
Taarifa ya TMA inaonesha kuwa hadi kufikia saa 3:00 asubuhi ya leo, vituo vya Same, Morogoro na Tabora vilirekodi mvua kubwa zilizozidi milimita 50 ndani ya saa 24, huku Same ikiongoza kwa milimita 94.5, ikifuatiwa na Morogoro (milimita 58.6) na Tabora (milimita 55.4).
Vituo vingine vilivyopima mvua ni pamoja na Hombolo (milimita 49.5), Kibaha (milimita 43.6), Dodoma (milimita 36.6) na Iringa (milimita 35.6), viwango vinavyoashiria kuendelea kwa mvua za wastani hadi kubwa katika maeneo mengi.
Katika Barabara Kuu ya Morogoro–Iringa, eneo la Mama Marashi hadi Mikumi, mvua hizo zimesababisha maporomoko ya mawe na tope kurundikana barabarani, hali iliyosababisha usumbufu wa usafiri wa magari.
Kwa ujumla, Serikali imeeleza kuwa inaendelea na jitihada za kurejesha huduma za usafiri na umeme katika hali ya kawaida, huku ikihakikisha usalama wa wananchi na miundombinu muhimu.
Kwa mtazamo wa hali ya hewa, TMA imetabiri kuwa mifumo iliyopo itaendelea kuimarika na kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara kesho tarehe 29 Desemba 2025.
TMA imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa wataalam ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizi.








