Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Media, Dodoma
Baadhi ya wananchi wa Jiji la Dodoma wameendelea kutoa maoni yao kuhusu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyohutubia Taifa kuaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka 2026, wakieleza matarajio yao mapya hususan katika kuimarishwa kwa ustawi wa wajasiriamali wadogo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Januari 2, 2026, wakazi wa Nzuguni B wamesema hotuba ya Rais imewapa matumaini mapya, lakini wakasisitiza umuhimu wa ahadi hizo kutafsiriwa kwa vitendo ili kugusa maisha ya wananchi wa kawaida wanaojitafutia kipato kupitia biashara ndogondogo.
Arafa Mhindi, mkazi wa Nzuguni B Mtaa na mjasiriamali pamoja na fundi wa kushona, amesema kuwa licha ya juhudi za serikali kutambua mchango wa wajasiriamali, changamoto zilizopo bado ni kubwa na zinahitaji ufumbuzi wa haraka.
Amesema gharama za kodi na leseni bado ni mzigo mkubwa kwa wajasiriamali wadogo, ikizingatiwa kuwa biashara nyingi ndogondogo hufanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine mtu hufanya kazi kwa mwezi mzima bila kupata faida.
Akirejea hotuba ya Rais Samia, Arafa amesema matarajio yao makubwa ni kuona mikopo inayotolewa na serikali, ikiwemo mikopo ya Mama Samia na ile ya asilimia 10 kupitia halmashauri, inawafikia walengwa halisi hususan wanawake na vijana wa chini.
Arafa ameongeza kuwa licha ya kuzunguka kwa muda mrefu kwa watendaji mbalimbali kufuatilia mikopo hiyo, bado hawajapata mafanikio, hali inayokatisha tamaa wajasiriamali wengi wanaotamani kukuza biashara zao.
Katika upande wa miundombinu, amesema barabara za maeneo ya Nzuguni B ni mbovu, zikiwa na makorongo na madimbwi, hali inayosababisha gharama kubwa za usafiri na ugumu wa kufika mjini kupata huduma muhimu ikiwemo matibabu na masoko ya bidhaa zao.
Hata hivyo, ameipongeza serikali kwa jitihada za kuboresha upatikanaji wa maji, akisema changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa na imewasaidia wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Sarah Nzunda, mkazi wa Nzuguni B, amesema hotuba ya Rais imegusia kwa ujumla masuala ya maendeleo, lakini changamoto za mitaji na miundombinu bado zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali wadogo, hasa katika kipindi cha masika.
Amesema barabara zilizojaa makorongo na ukosefu wa madaraja husababisha wafanyabiashara kushindwa kufika sokoni au maeneo ya kuchukua bidhaa, hali inayosababisha kupoteza siku nzima bila kufanya biashara.
Mkazi mwingine wa Nzuguni, Rashid, amesema maisha bado ni magumu lakini wameendelea kujitahidi kwa kujiunga katika vikundi vya kijamii ili kupata mitaji ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao.
Amesema ana matumaini kuwa katika mwaka 2026, serikali itaimarisha usimamizi wa mikopo ya wajasiriamali ili iwe chachu ya maendeleo badala ya kuwa chanzo cha malalamiko, huku akiwahimiza vijana kuepuka makundi yasiyo sahihi na kujikita katika shughuli halali za kiuchumi.
Kwa ujumla, wananchi wa Nzuguni B wamesema wanaupokea mwaka 2026 wakiwa na matumaini mapya baada ya hotuba ya Rais Samia, lakini wakisisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi hizo ndio utakaopima mafanikio halisi ya dhamira ya serikali ya kuwainua wajasiriamali wadogo nchini.






