

Mahakama Kuu ya Venezuela imemteua Makamu wa Rais Delcy Rodríguez kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo, kufuatia tangazo la Marekani kwamba Rais Nicolás Maduro amezuiliwa na vikosi vya Marekani na kuhamishiwa nchini humo.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama hiyo ulioripotiwa na Reuters Jumapili, Rodríguez atachukua majukumu ya Rais Maduro ili kuhakikisha mwendelezo wa serikali, kusimamia shughuli za dola na kuongoza masuala ya ulinzi wa taifa wakati wa kile kilichoelezwa kuwa “kutokuwepo kwa lazima” kwa rais.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu imesema mfumo wa kisheria umeanzishwa kwa dharura ili kulinda taasisi za serikali na uhuru wa taifa, ikisisitiza kuwa uhamisho wa madaraka ni wa muda na unalenga kudumisha utaratibu wa kikatiba nchini humo.
Mahakama imeongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia ombwe la madaraka na kuhakikisha shughuli za serikali zinaendelea bila kuvurugika.
Maafisa wa Marekani wamesema vikosi maalum vya nchi hiyo vilitekeleza operesheni ya alfajiri nchini Venezuela kwa agizo la Rais wa Marekani Donald Trump, huku kukiripotiwa milipuko na ongezeko la shughuli za kijeshi katika maeneo kadhaa ya mji mkuu, Caracas.
Trump amedai kuwa Maduro alikamatwa wakati wa operesheni hiyo na kuhamishiwa New York ili kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazohusiana na biashara ya dawa za kulevya na makosa mengine. Hata hivyo, mamlaka za Venezuela zimepinga vikali hatua hiyo, zikisema haina uhalali wa kisheria.
Marekani imekuwa ikiishutumu Venezuela kwa muda mrefu kwa kuendesha kile inachokiita “nchi ya biashara ya dawa za kulevya”, madai yaliyosababisha vikwazo vikali vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Caracas, sambamba na kuunga mkono juhudi za upinzani kuleta mabadiliko ya kisiasa.
Maduro, aliyeingia madarakani mwaka 2013 baada ya kifo cha Rais Hugo Chávez, amekuwa akikanusha mara kwa mara tuhuma hizo, akizitaja kama njama za kisiasa za Marekani.
Mahakama Kuu ya Venezuela imekuwa ikikosolewa vikali na wapinzani na jumuiya ya kimataifa, wakidai imeegemea upande wa chama tawala. Mtazamo huo umekuwa chanzo cha migogoro kuhusu uhalali wa maamuzi yake katika migogoro ya kisiasa ya awali nchini humo.
The post Delcy Rodríguez Aapishwa Kuongoza Venezuela kwa Muda appeared first on Global Publishers.




