*Huko kuna sheria za kimila mtu anakufanya chochote na serikali haiingilii.
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Media, Dodoma
Dereva wa magari ya mizigo, Juma Maganga, aliyekuwa ameshikiliwa na vyombo vya sheria nchini Sudan Kusini, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kila kitu.
Maganga ameyasema hayo Januari 3, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili nyumbani kwake jijini Dodoma, akitokea nchini Sudan Kusini alikokuwa ameshikiliwa kufuatia ajali iliyotokea Februari 14, 2025, ambapo akiwa dereva wa gari kubwa alimkonga mwanajeshi mmoja aliyepoteza maisha.
Amesema kuwa nchini Sudan Kusini kukosekana kwa amani kumesababisha wananchi kuongozwa zaidi na sheria za kimila badala ya sheria za nchi, hali inayosababisha kila mtu kuwa na mamlaka yake binafsi bila maamuzi ya serikali.
Aidha, amesema hali hiyo husababisha kukosekana kwa utulivu kwani kila mtu anajiamulia jambo analotaka kufanya bila kuzingatia mamlaka ya dola.
Kwa upande wake, Kado Shaban, Afisa Usafirishaji wa Abiria maarufu bodaboda Stand ya Nanenane jijini Dodoma, amesema amani imechangia kurahisisha maisha na shughuli za kiuchumi.
Amesema vijana wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, kumuomba Mungu na kuepuka vurugu, akibainisha kuwa kipindi cha kukosekana kwa amani biashara nyingi zilisimama na gharama za maisha kuongezeka, ikiwemo bei ya mafuta.
Naye Hamisi Juma, Afisa Usafirishaji wa Nzuguni Boda na mkazi wa Dodoma, amesema amani ndiyo nguzo ya maisha ya binadamu na maendeleo ya taifa.
Amebainisha kuwa bila amani watu hushindwa kufanya kazi, kusafiri na kuendeleza maisha yao ya kila siku, akisisitiza kuwa haki na amani haviwezi kutenganishwa kwani kukosekana kwa haki husababisha migogoro na vurugu.
Ameongeza kuwa baadhi ya vijana huingia katika makundi yenye nia mbaya kutokana na vishawishi, huku akiwataka vijana kujitambua, kujua walikotoka na wanakokwenda kwa kuwa wao ndiyo taifa la baadaye.
Aidha, amesema vijana wengi wameingia katika kazi za usafirishaji si kwa sababu hawajasoma, bali kutokana na uhaba wa ajira, wakichagua kujitafutia kipato halali ili kuepuka uhalifu.
Pia amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha mazingira ya kazi kwa waendesha bodaboda Nzuguni, ikiwemo ujenzi wa kituo chao, huku akieleza matumaini kuwa changamoto za barabara zitaendelea kufanyiwa kazi.




