Na Sabiha Khamis Maelezo 08.01.2026
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar inaendeleza jitihada katika kukuza uchumi na kuhakikisha wananchi na wafanyabiashara wa Zanzibar Ahuduma nzuri ikiwemo kuimarisha miundombinu ya usafiri wa umma.
Ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi kituo cha mabasi ya umeme Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa muendelezo wa shamrashamra za kutimiza miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) imeamua kuwekeza katika miradi mbalimbali ya vituo vya kisasa vya mabasi ya abiria ili wananchi wapate sehemu maalum za kupanda na kushuka kwenye usafiri bila ya usumbufu.
Amefafanua kuwa mipango miji ni kichocheo cha maendeleo ambayo huongeza ajira ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza uchumi wa nchi katika kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha amesfahamisha kuwa mkakati wa Serikali kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuwawekea miundombinu wezeshi ya kurahisisha usafiri kwa wananchi ili waweze kufanya shughuli za maendeleo kwa wakati na urahisi.
Ameziomba taasisi zinanzohusika na huduma za usafiri kuendelea kutoa mafunzo na elimu kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya usafiri ili kuenda sambamba na kutambua mabadiliko hayo.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Hamad Omar Bakar amesema kuanzishwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ZSSF umekuwa muhimili muhimu katika kukuza uchumi wa nchi katika kujikita katika miradi ya maendeleo ambayo inatija kwa taifa ikiwemo ujenzi wa vituo vya mabasi.
Amesema kuwa kumalizika kwa kituo hicho kutawawezesha vijana wengi watapata ajira hali ambayo itakayopelekea kuinua uchumi wa nchi na wananchi kujikimu kupitia miradi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugezi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ZSSF Nassor Shaaban Ameir amesema kuwa ZSSF imetekeleza mradi huo kwa vitendo kwa kufuata maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar katika sekta ya usafiri wa umma.
Amefahamisha kuwa ZSSF imeendelea kubuni namna ya kuboresha huduma ya usafiri wa umma kwa kujenga vituo vya mabasi na kubadilisha mfumo wa vyombo vya usafiri Zanzibar.
Amesema mradi huo umeanza kutekelezwa baada ya makubaliano na Mkandarasi Emirate Co.ltd Aprili 25, 2025 ambapo mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji wake ambao unajumuisha eneo la maegesho ya mabasi 50 kwa wakati mmoja, mabasi madogo yanayoelekea Mji Mkongwe, Ofisi za kutoa huduma za kituo, Sehemu za kukatia tiketi. Sehemu ya kusalia wanawake, sehemu za huduma za kijamii kwa wanawake, wanaume na watu wenye mahitaji maalum pamoja na kiwanja cha mpira wa miguu.






