Na John Bukuku – Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania nje ya nchi, ambapo jumla ya vijana 1,432 tayari wamepata ajira na wameshasafiri kwenda kufanya kazi katika mataifa mbalimbali, hatua inayotajwa kuwa matokeo ya maboresho ya mifumo ya ajira na diplomasia ya kazi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mhe. Deus Sangu, wakati akizungumza katika hafla ya kuwaaga vijana 109 wanaoelekea kufanya kazi nje ya nchi, iliyofanyika leo katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Waziri Sangu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya ajira ndani na nje ya nchi, ikiwemo kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ajira, kuongeza ulinzi wa kisheria kwa wahamiaji wa kazi pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana kabla ya kuondoka kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Amesema jitihada hizo zimekwenda sambamba na kukuza ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na nchi mbalimbali zinazopokea wafanyakazi, hatua inayoongeza uaminifu na kulinda maslahi ya vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.
“Ninatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyofanya ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kwani mahusiano hayo ndiyo chanzo cha fursa hizi zote za ajira kwa vijana wetu,” amesema Waziri Sangu.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, hususan wakala wa ajira, ili kuhakikisha vijana wanapata fursa zaidi za ajira kwa uwazi, usalama na kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo iliyopo.
Waziri Sangu amebainisha kuwa hadi sasa vijana 1,323 tayari wamekwishasafiri kwenda kufanya kazi nje ya nchi kupitia uratibu wa Serikali kwa kushirikiana na wakala binafsi wa ajira, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia vijana 1,432, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhusu ajira kwa vijana ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema bado zipo fursa zaidi ya ajira 8,000 kwa vijana wa Kitanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi, fursa ambazo zitaendelea kupatikana kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Zuhura Yunus, amesema ajira nje ya nchi ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa utekelezaji wake unazingatia kikamilifu sera, sheria na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kwa usalama na tija.
Amesisitiza vijana kuchangamkia fursa hizo kwa kuzingatia taratibu rasmi, akibainisha kuwa ajira nje ya nchi ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.








