Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya akiongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa wakati wa kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo katika chuo hicho.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa wakimaliza Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya wakati akitoa hotuba yake
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya akikabidhi kiasi cha shilingi milioni mbili kwa uongozi wa chuo kikuu cha Iringa zilizotolewa na Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, kwa ajili ya kuwaunga mkono wanafunzi hao.
Na Fredy Mgunda, Iringa.
Wanafunzi wa vyuo vikuu wametakiwa kujiepusha na ndoa za rejareja,makundi ya hovyo yenye viashiria vya kuharibu masomo na maisha kwa wanafunzi wenye ndoto ya kuja kulitumikia taifa la Tanzania na nje ya Tanzania.
Akizungumza wakati kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Iringa,Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya alisema kuwa wanafunzi wanapaswa kuepukana na ndoa za rejareja, makundi ya hovyo na kuwa wazalendo kwa ajili ya maisha yao.
Dkt Msowoya amesema baadhi ya wanafunzi hujikuta wakitumbukia kwenye ndoa za rejareja na kusahau lengo la masomo kutokana na tamaa za kifedha na kuishi maisha mazuri chuo jambo ambalo limekuwa likipoteza dira ya masomo kwa wanafunzi wengi.
“Najua mna miaka zaidi ya 18 hivyo sio watoto Kwa mujibu wa kawaida lakini je, ndoa ndiyo imekuleta chuoni? Wazazi wako wanajua umeoa au kuolewa huku?” amesema na kuongeza, Dkt Msowoya
“Niliwahi kufanya utafiti kuhusu maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu nikagundua wengi wanaishi na wenza ilhali familia zao hazijui. Hii ni hatari,”
Dkt. Msowoya aliwahimiza wanafunzi kuipenda nchi yao, kusoma kwa bidii na kuepuka makundi yenye viashiria hasi katika masomo na maisha kwa ujumla.
Katika hafla hiyo, alitoa mchango wa shilingi milioni mbili (2,000,000) zilizotolewa na Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, kwa ajili ya kuwaunga mkono wanafunzi hao.






