Na John Walter-Mbulu
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Dkt. Emmanuel Nuwas, ameendelea na ziara yake ya kuwatembelea na kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao Bungeni.
Katika ziara hiyo, Dkt. Nuwas amesisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu, kama alivyowaahidi wakati wa kampeni.
Akiwa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, Mbunge huyo ametumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti.
Ameeleza kuwa kipindi hiki cha mvua ni fursa adhimu kwa wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi ili kulinda mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Nuwas amekuwa akipanda miti katika kila eneo analopita kama mfano wa kuigwa, huku akiwahimiza wananchi kuiga hatua hiyo kwa kupanda miti katika mashamba, makazi na maeneo ya taasisi za umma.
Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na una mchango mkubwa katika kuboresha afya na maisha ya jamii kwa ujumla.
Katika ziara yake hiyo, Mbunge Dkt. Emmanuel Nuwas anatembea na kauli mbiu isemayo “Mazingira ni afya, panda miti tunza mazingira”, kauli mbiu inayolenga kuamsha ari ya wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo.





