Na OWM- TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Dkt. Jafar Seif, amewaelekeza wakuu wa mikoa yote nchini kuratibu na kutekeleza mpango Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma na hamasa kwa wananchi ili waweze kujiunga na mpango huo.
Dkt. Seif ametoa maelekezo hayo katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete – JKCC mapema leo Januari 23, 2026 Jijini Dodoma, kwa niaba ya waziri wa Nchi OWM- TAMISEMI wakati akifunga rasmi kikao kazi cha kujadili kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Ameongeza kuwa Wakuu wa Mikoa wana jukumu la kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa na pia kusimamia maelekezo ya kuwa na mfumo mmoja unaosomana katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Dkt. Seif ameelekeza pia kuwa ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote iwe ya kudumu katika Vikao vya Kamati za Ushauri vyala Mikoa (RCC) na Wilaya (DCC) na kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mikoa yote vinasajiliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ili viweze kutoa huduma za Bima ya Afya kwa Wote.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI Prof. Tumaini Nagu ameeleza kuwa TAMISEMI iko tayari kutekeleza na kusimamia mpango huo ili wananchi waweze kunufaika kwa kupata huduma bora hususani wale wasio na uwezo.
Prof. Nagu ameongeza kuwa Wizara hiyo pia itasimamia maelekezo kwa kuhakikisha mifumo inasomana ili kuwezesha wananchi kupata huduma za Bima ya Afya kwa Wote.
Awali akifungua kikao kazi hicho, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaanza kwa awamu na mwanachama atapaswa kuchangia Shilingi 150,000 ambayo inahusisha mke na mume pamoja na wategemezi wanne.
Amesema katika awamu ya kwanza kitita cha huduma muhimu za Bima ya Afya kwa Wote kitaanza tarehe rasmi tarehe 26 Januari 2026 na kitawahusisha pia watoto, wanawake na wazee wasiojiweza ambao watagharamiwa na Serikali.






