Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema kuwa wizara hiyo haitavumilia vitendo vya ukiukwaji wa maadili na nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa ardhi dhidi ya wananchi wanaotafuta huduma katika ofisi za umma.
Akizungumza January 23,2026 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi nchini, Dkt. Akwilapo amebainisha kuwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya ardhi ni msingi muhimu wa kutoa huduma bora na kupunguza migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, amewataka watumishi wa sekta hiyo kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa wazi na wa haki kuhusu malalamiko ya wananchi, sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu ya masuala ya ardhi kwa jamii ili kuongeza uelewa na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi (Mb), Caspar Muya, amesema kuwa maadili, uwajibikaji na utunzaji wa siri za serikali ni nguzo muhimu katika utumishi wa umma. Aidha amebainisha kuwa kila mtumishi anatakiwa kuacha alama chanya anapostaafu au anapobadilishiwa majukumu, kwa kuzingatia misingi ya utumishi uliotukuka.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kuwa watumishi wa sekta ya ardhi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia utu, weledi na heshima kwa wananchi. Aidha amesisitiza kuwa changamoto za sekta ya ardhi zinapaswa kutatuliwa kwa wakati, huku akihimiza wananchi kupata majibu stahiki ya migogoro yao katika maeneo husika bila usumbufu usio wa lazima.
Kikao kazi hicho kililenga kuimarisha utendaji kazi, maadili na uwajibikaji kwa watumishi wa ardhi nchini, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.






