Na. John Bukuku – Dar es Salaam
MKOA wa Dar es Salaam umefanikiwa kuvuka lengo la utoaji wa huduma za upasuaji wa mabusha, matende na ngirimaji baada ya mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kupimwa na kutibiwa kupitia kambi maalum ya kitaifa inayoendelea katika Kituo cha Afya Yombo Kilakala.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali imefanikiwa kufikia na hata kuvuka lengo la awali la kuwahudumia wananchi 500, baada ya zaidi ya wananchi 1,300 kujitokeza kupimwa kufuatia kampeni ya uhamasishaji na elimu kwa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 25, 2026, Dkt. Magembe amesema kambi hiyo ilianza Januari 5 na inatarajiwa kukamilika Januari 30, 2026, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi waliokumbwa na magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambayo huathiri kwa kiwango kikubwa maisha na uwezo wa kufanya kazi.
Amesema kuwa kati ya wananchi waliojitokeza, wagonjwa 668 wamegundulika kuwa na mabusha na ngirimaji, na kati yao wagonjwa 457 tayari wamefanyiwa upasuaji.
Dkt. Magembe amesema upasuaji huo unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa na utaalamu wa hali ya juu, ambapo wagonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa ya usingizi wa sehemu (local anesthesia), hali inayowawezesha kurejea nyumbani siku hiyohiyo baada ya kufanyiwa upasuaji.
Amesema kwa siku, wagonjwa takribani 50 hufanyiwa upasuaji, huku vituo vya upasuaji vikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa watano hadi sita kwa wakati mmoja, kwa kuzingatia taratibu zote za usafi na udhibiti wa maambukizi.
Aidha amebainisha kuwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hufuatiliwa kwa karibu baada ya matibabu, ambapo hurejea kituoni baada ya wiki moja au mbili kwa ajili ya tathmini ya maendeleo ya afya zao.
Dkt. Magembe amesema kambi hiyo pia inatumika kama jukwaa la kujenga uwezo kwa watumishi wa sekta ya afya kutoka ngazi mbalimbali, wakiwemo wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), hospitali za rufaa za mikoa pamoja na vituo vya afya vya ngazi ya chini.
Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa hata baada ya kampeni, huduma za upasuaji wa magonjwa hayo zinaendelea kutolewa katika vituo vya afya kwa ufanisi.
Aidha amebainisha kuwa kupitia zoezi hilo, Serikali imegundua wagonjwa takribani 400 wenye magonjwa mengine yasiyohusiana na mabusha wala ngirimaji, ikiwemo henia, na kwamba Serikali imeamua kuwahudumia pia wananchi hao.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Hospitali ya Taifa Muhimbili imeweka utaratibu wa kuhakikisha wagonjwa wote waliogundulika wanapata huduma stahiki.
Dkt. Magembe amesema utekelezaji wa zoezi hilo umewezeshwa na Serikali baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa shilingi bilioni nne kwa ajili ya kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele nchini.
Amebainisha kuwa Serikali imeanzisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa urahisi, kwa gharama nafuu na kwa ubora unaostahili, huku wananchi wasio na uwezo wa kipato wakigharimiwa na Serikali.
Aidha amesisitiza kuwa magonjwa ya mabusha, matende na ngirimaji husababishwa na vimelea vinavyoenezwa na mbu, na kwamba usafi wa mazingira ni muhimu katika kuzuia magonjwa hayo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Mohammed Mang’una, amesema mafanikio ya kampeni hiyo yametokana na uhamasishaji uliofanyika katika masoko makubwa na maeneo ya usafiri wa umma, hali iliyopelekea ongezeko kubwa la mwitikio wa wananchi.
Amesema kambi ya Mkoa wa Dar es Salaam itaendelea hadi Januari 30, 2026, na wananchi wamehimizwa kujitokeza mapema kwa ajili ya uchunguzi na upangaji wa tarehe za upasuaji, huku huduma zikiendelea hata baada ya kukamilika kwa kambi hiyo.






