Kibaha, Pwani | Januari 27, 2026 – Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amesema wilaya hiyo inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kulinda na kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaendana na utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza leo wakati wa zoezi la upandaji miti 200 kati ya 2,000 iliyopangwa kupandwa katika Shule ya Sekondari Msangani Two, Manispaa ya Kibaha, Simon alisema wilaya hiyo inalenga kuvutia wawekezaji wanaozalisha nishati safi ikiwemo gesi, sambamba na kuweka mazingira rafiki kwa taasisi na wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa mazingira.
Alisema mikakati hiyo inaendana na dira ya taifa ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda rasilimali za asili na kuhifadhi vyanzo vya maji
“Hatua tunazochukua zinalenga kuhakikisha maendeleo yanayopatikana leo hayaharibu mustakabali wa vizazi vijavyo,” alisema Simon.
Tukio hilo limefanyika kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambao umeendelea kutoa miche ya miti, elimu ya uhifadhi wa mazingira na ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kudumu.
Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TFS, SACC Mathew Ntilicha, alisema wakala huo unaendelea kushirikiana na taasisi za elimu na jamii katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Uongozi wa Shule ya Sekondari Msangani Two ulieleza kuwa umejiwekea mkakati wa kupanda zaidi ya miche 20,000 ya miti kila mwaka, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya shule na jamii inayozunguka eneo hilo.
Mkakati huo ulielezwa kupitia risala iliyosomwa na mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, Janeth Victor, ambaye alisema shule tayari imeanza utekelezaji kwa kununua viriba 32 vya miche ya miti ya matunda na kivuli, hatua inayolenga kuimarisha uoto wa asili, mazingira ya kujifunzia na kuchangia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Uongozi wa shule uliiomba serikali pamoja na wadau wa mazingira kuunga mkono juhudi hizo, huku ukipendekeza kuanzishwa kwa ushindani wa upandaji miti kati ya shule ili kuongeza hamasa ya utunzaji wa mazingira na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili.






