Na Sophia Kingimali
Baadhi ya wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wametoa wito mzito kwa vijana wa kizazi cha Gen Z kudumisha upendo na amani, wakisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Januari 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hafla hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Vijana Innovation na kuratibiwa na Taasisi ya Together for Samia, sambamba na maombi maalum ya kumuombea Rais Dkt. Samia aendelee kuiongoza Tanzania kwa amani na utulivu.
Katika hafla hiyo, wazee na vijana wameahidi kushirikiana kwa karibu katika kudumisha upendo, mshikamano na amani kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Wazee hao wamesema kuwa Tanzania imebarikiwa amani kubwa inayotamaniwa na mataifa mengi duniani, hivyo vijana wanapaswa kuwa walinzi wakuu wa tunu hiyo kwa kuishi kwa upendo, mshikamano na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Akizungumza kwa niaba ya wazee, Bi. Sophia amesema kuwa wazee wataendelea kuliombea Taifa, huku akisisitiza kuwa vijana nao wana wajibu wa vitendo katika kuhakikisha amani inatawala, kwani bila amani hakuna maendeleo wala ustawi wa kweli.
“Tanzania ni nchi ya amani, tusivuruge amani tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Amani hii inatafutwa na mataifa mengi. Vijana, tusaidieni kuilinda na kuikuza,” amesema, huku akiwataka vijana kujishughulisha na kazi na kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Nathaniel Maseke, amesema kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita unaonesha dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana kupitia elimu, ujuzi na fursa za kiuchumi.
Ameeleza kuwa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika maeneo mbalimbali nchini umeongeza fursa kwa vijana kujifunza ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Maseke ameongeza kuwa Rais Samia amefanya mageuzi makubwa katika sekta muhimu zikiwemo afya, nishati, elimu na miundombinu, hatua iliyochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha, amesema kuwa msisitizo wa Rais katika maridhiano, umoja na amani umeweka mazingira salama kwa vijana kushiriki shughuli za maendeleo bila hofu.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovation, Dorcas Richard, amesema Serikali imeendelea kufungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hali inayoongeza ajira na fursa za biashara kwa vijana.
Amebainisha kuwa mikopo ya vijana yenye riba ya asilimia mbili imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo, huku vijana wengi tayari wakinufaika na sera hizo. Amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kufungua njia za mafanikio kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa niaba ya vijana, Ridhiwani Chakachaka na Hajrati Miraji wamesema kuwa juhudi za Rais Samia zimewezesha vijana kueleza changamoto na malalamiko yao kwa njia ya amani na kupata suluhu bila migogoro.
“Kuanzishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana kumeongeza sauti na nafasi ya vijana katika maamuzi ya Taifa, jambo lililotupa matumaini mapya ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo,” amesema Chakachaka.
Ameongeza kuwa vijana wanamuunga mkono Rais kwa asilimia 100 kwa kutambua mchango na umuhimu wao pamoja na kuwa kiongozi anayejali mustakabali wa kizazi kijacho.
Kwa upande wa wanawake, Hajira amesema kuwa uongozi wa Rais Samia umeleta hamasa kubwa kwa wanawake kushiriki katika uongozi na shughuli za kiuchumi, kijamii na kiafya, hali inayochangia ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla.






