NA DENIS MLOWE IRINGA
DIWANI wa Kata ya Kwilosa iliyoko manispaa ya Iringa, Hamid Mbata, ameongoza uzinduzi rasmi wa kampeni ya upandaji miti katika kata hiyo, ikiwa ni hatua madhubuti ya kutunza mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tukio hilo limehudhuriwa na wakazi wa maeneo mbalimbali ya kata hiyo, wakiwemo viongozi wa mitaa, mashirika ya kijamii na wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari walioshiriki katika maeneo ya shule za kata hiyo.
Katika hotuba yake, Diwani Mbata alisisitiza kuwa upandaji miti si tukio la siku moja, bali ni jukumu la kudumu linalohitaji ushirikiano wa wananchi wote. Alisema kuwa kwa muda mrefu kata ya Kwilosa imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uharibifu wa mazingira, jambo linalohitaji hatua za haraka ili kuzuia madhara makubwa zaidi.
Mbata alieleza kuwa kampeni hiyo imepangwa kufanyika kila mwaka katika mitaa yote katika kata, ikiwa na lengo la kupanda maelfu ya miche ya miti ya matunda, kivuli na miti ya asili.
Aliongeza kwa kuanza wameanza na miti zaidi ya 5000 na mitaa itapewa jukumu la kuisimamia miche hiyo hadi ikue na kuwa miti imara itakayowanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, alitoa pongezi maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuhimiza na kutekeleza mikakati ya kitaifa ya kuhifadhi mazingira.
Alisema kampeni ya Kwilosa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa taifa lenye mazingira salama, safi na endelevu.
Wananchi walioshiriki katika uzinduzi huo walionesha hamasa kubwa, huku wengi wakisema kuwa ni mara ya kwanza kuona kampeni ya mazingira ikiratibiwa kwa kiwango hicho katika eneo lao.
Baadhi ya wazazi waliwahimiza watoto wao kushiriki kikamilifu, wakisema elimu ya mazingira lazima ianze mapema ili kuijenga jamii yenye uelewa na uwajibikaji.
Shule mbalimbali za kata ya Kwilosa pia zilipata nafasi ya kupanda miti katika maeneo ya shule, ikiwa ni sehemu ya kuunganisha juhudi za elimu na uhifadhi wa mazingira. Walimu walisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo umuhimu wa miti na namna ya kuitunza.
Uzinduzi huo umeacha ujumbe mzito kwa wakazi wa Kwilosa kuwa mazingira ni utajiri na uhai wa jamii huku diwani Mbata aliwahimiza wananchi kuendeleza kampeni hiyo kwa moyo mmoja, akisisitiza kuwa kata hiyo ina uwezo wa kuwa mfano bora kitaifa endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake katika utunzaji wa mazingira.





