

Iran imesisitiza kwa msimamo mkali kuwa haitaacha kurutubisha uranium, hata kama italazimika kukabiliana na vita, kauli inayozidisha mvutano wa kidiplomasia na kijeshi kati ya Tehran na Washington pamoja na washirika wake.
Akizungumza katika jukwaa la kisera jijini Tehran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema suala la urutubishaji wa uranium ni haki ya kitaifa isiyojadiliwa, na kwamba Iran imekuwa ikilipa gharama kubwa kwa miaka mingi kwa kusimamia kile inachodai kuwa mpango wake wa nyuklia wa amani.
“Iran imelipa gharama kubwa sana kwa ajili ya mpango wake wa nyuklia wa amani na kwa ajili ya urutubishaji wa uranium.
Tumekabiliwa na vikwazo, vitisho na mashinikizo ya kila aina,” amesema Araghchi.
“Kwa nini tunasisitiza sana kuhusu urutubishaji na tunakataa kuachana nao hata kama vita italazimishwa juu yetu? Ni kwa sababu hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kutuamuru au kutuambia namna ya kuendesha masuala yetu ya ndani.”
Kauli hiyo imekuja siku chache tu baada ya Araghchi kukutana na mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff, nchini Oman. Mkutano huo ulitajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano, lakini kauli za pande zote zinaonyesha kuwa tofauti kubwa bado zipo, hasa kuhusu masharti ya mazungumzo mapya ya nyuklia.

Araghchi pia amesema Iran haioni tishio katika ongezeko la uwepo wa kijeshi wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi, akidai kuwa Tehran imezoea vitisho vya aina hiyo kwa miongo kadhaa.
“Upelekaji wao wa kijeshi katika eneo hili haututishi. Iran ina uwezo wa kujilinda na kulinda maslahi yake,” amesema.
Kwa upande wa Marekani, Rais Donald Trump ameendelea kuchukua msimamo mkali dhidi ya Iran, akitishia mara kwa mara kutumia nguvu za kijeshi ili kuilazimisha Tehran kufikia makubaliano mapya kuhusu mpango wake wa nyuklia. Marekani pia imeongeza idadi ya wanajeshi, manowari na vifaa vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
The post Iran Yasema Haitaacha Kurutubisha Uranium Hata Itangazwe Vita appeared first on Global Publishers.




