

Watu watatu wamefariki dunia usiku wa kuamkia Februari 8, 2026, baada ya kuhusika katika majibizano ya risasi na Askari Polisi katika Mtaa wa NMB, Kata ya Malambo, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane na nusu usiku, baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa za watu waliokuwa wakivunja milango ya jengo la Simiyu Money Services, linalotoa huduma za miamala ya fedha kwa kampuni za simu na taasisi za kifedha.
Baada ya taarifa hiyo, Kikosi Maalum cha Kuzuia na Kupambana na Uhalifu kilifika katika eneo la tukio. Inadaiwa kuwa watuhumiwa walipobaini uwepo wa Polisi walianza kufyatua risasi, hali iliyosababisha Askari Polisi kujibu mashambulizi hayo.
Katika majibizano hayo, watuhumiwa watatu walijeruhiwa na baadaye walifariki dunia wakiwa njiani kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Askari Polisi walifanikiwa kukamata silaha moja aina ya AK-47 pamoja na risasi nane zilizokuwa ndani ya magazini. Aidha, katika upekuzi, walikutwa na shilingi mia tatu za Kenya, noti moja ya shilingi tano ya Misri, tiketi ya safari kutoka Migori kwenda Sirari pamoja na tiketi za kutoka Sirari hadi Lamadi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeendelea kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu mapema ili kusaidia kudhibiti vitendo vya kihalifu katika jamii.
The post Majambazi Watatu Wauawa Simiyu Wakifyatuliana Risasi na Polisi appeared first on Global Publishers.




