Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Ujenzi kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara iliyosainiwa kabla ya kuanza mipya ili kuleta.
Akizungumza katika ziara yake wilayani Kilindi mkoani Tanga Dkt. Mwigulu amesema kukamilika kwa miradi iliyosainiwa kutaiwezesha Serikali kuwa na miradi inayotekelezeka kwa wakati na kuiwezesha Serikali kuisimamia vizuri.
“Hakikisheni mnakamilisha ujenzi wa barabara ya Handeni-Mafuleta- Kileguru Km 50, kwanza kabla hamjaanza sehemu ya Kileguru – Songe km 63”, amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema Serikali imepanga kuijenga kwa lami barabara yote ya Handeni-Kiberashi- Kwamtoro-Singida km 434.33 ili kuiongezea tija bandari ya Tanga.
Amesema Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Bandari (TPA) wako katika hatua za mwisho za kuijenga barabara hiyo kwa ubia (PPP).
Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha kwa njia fupi bandari ya Tanga na mikoa ya kati na Kanda ya ziwa.
“Tumejipanga kuzijenga kwa lami barabara za Songe-Chakwale-Ngilori na Songe- Vyadigwa-Mziha-Turiani ili kuifungua wilaya ya Kilindi na mkoa wa Morogoro kwa barabara za lami na hivyo kuchochea uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo”, amesema Eng. Kasekenya.
Waziri Mkuu Nchemba yuko mkoani Tanga katika ziara ya siku tatu kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.





