………..
Viongozi Chemba wakumbushwa uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza majukumu yao
Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba iliyopo mkoani Dodoma wamekumbushwa kufanya kazi kwa pamoja huku wakisisitizwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kauli hiyo imesemwa tarehe 14 Februari, 2026 na Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma Bi. Jasmin Awadhi wakati akitoa mafunzo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Viongozi wa Halmashauri hiyo.
“Kufanya kazi kwa mazoea kumechangia Taasisi nyingi kutofikia malengo yao, na hii ni kutokana na watu wachache kushikilia majukumu mengi kwa wakati mmoja na kuwanyima fursa wengine kuonyesha uwezo wao,’’ alisema Bi. Jasmin.
Aidha Bi. Jasmin ametumia mafunzo hayo kuwakumbusha Viongozi hao kufanya kazi kwa huruma, maelewano na kutumia njia sahihi za mawasiliano ili kuondoa sintofahamu katika utendaji wao na hatimaye kuleta maendeleo katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla.
“Mawasiliano ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku, hivyo kama njia hii haitatumika vyema hatuwezi kupiga hatua katika kutatua changamoto za wananchi maana kila kila mmoja atakua anafanya lake, hivyo msingi mzuri wa mawasiliano ni tija katika uwajibikaji hasa kwa kufata chaneli nzuri katika kuwasiliana huko.’’ Alisema.
Kwa upande Diwani wa Kata ya Ovada ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Lebba amesema kuwa wao kama Viongozi wamepokea kwa mikono miwili mafunzo hayo maana miongoni mwao kuna Madiwani wengi wapya ambao walikua na upungufu katika kufahamu dhana nzima ya maadili.
“Mimi hii ni awamu ya pili kupata mafunzo haya, lakini Madiwani wengine ni wapya hivyo kwangu ni fursa kujikumbusha tena maana Kiongozi lazima uwe na maadili ili kuwatendea haki watu unaowaongoza,’’ alisema Mhe. Lebba.
Katika mafunzo mada mbali mbali ziliwasilishwa na wawezeshaji kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo Madiwani, Wakuu wa Vitengo na Idara wa Halmashauri hiyo walipata nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo.





