Katika kuboresha maeneo ya kuswalia kwa waumini wa Kiislamu katika Manispaa ya Musoma, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agness Mathew, amekabidhi busati za kufanyia ibada katika misikiti yote ya manispaa hiyo pamoja na tende, huku akiwaomba viongozi wa misikiti kuendelea kuwa sehemu ya kuwaunganisha Watanzania katika umoja.
Agness amekabidhi busati (zulia) hizo ambazo zitasaidia waumini kuswali katika mazingira safi, huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa namna yoyote itakayohitajika.
Awali, baadhi ya viongozi wa misikiti katika Manispaa ya Musoma wamepongeza hatua hiyo wakieleza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa marekebisho ya nyumba za ibada katika maeneo yao.
“Tunakushukuru sana kwa hiki; wengi wamekuwa wakisahau kukumbuka nyumba za ibada, lakini ulichokifanya tunakupongeza sana,” alisema Shekhe Aman Kapama, Shekhe wa Msikiti wa Nyamatare.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Nyabiti, alisema viongozi wa dini wana uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Watanzania na kuhakikisha mshikamano unaendelea miongoni mwa wananchi na viongozi wao.





