Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema kuwa VETA inaendelea kutoa fursa kwa vijana waliopata ujuzi bila vyeti rasmi kupitia mpango wa Urasimishaji wa Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL).
Amesema kuwa mpango huu unalenga kurasimisha ujuzi wa vijana mafundi waliopata mafunzo sehemu za kazi ili waweze kupata vyeti rasmi na hivyo kuongeza fursa za ajira na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi.
Ameyasema hayo Februari 16,2026 Jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba, Mji wa Serikali.
Aidha, amebainisha kuwa hadi Januari 2026, jumla ya wanagenzi 25,523 (wakiume 21,547 na wakike 3,976) wamenufaika na programu ya RPL, huku lengo la mwaka wa fedha 2025/2026 likiwa ni kurasimisha ujuzi wa jumla ya mafundi 30,000.
Pia ameongeza kuwa mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mama Samia ya Urasimishaji wa Ujuzi, inayolenga kurasimisha ujuzi kwa vijana 80,000 nchini kote ifikapo Juni 2027. Amesema kuwa hatua hii ni fursa muhimu kwa vijana waliopata mafunzo sehemu za kazi, kwani inawawezesha kupata vyeti rasmi, kushiriki kwenye zabuni, na kupata ajira rasmi.
Aidha, amebainisha kuwa VETA inatoa mafunzo kwa wajasiriamali kwenye sekta isiyo rasmi kupitia mpango wa Mafunzo Jumuishi ya Kukuza Ujasiriamali (INTEP), ambapo wajasiriamali 7,040 wamefaidika hadi sasa. Amesema kuwa mpango huu unalenga kuongeza umahiri wa vijana na wanawake katika shughuli zao za kiuchumi, huku ukichangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia ameongeza kuwa miradi mingine ya VETA inayolenga vijana na makundi maalum ni pamoja na YEFFA, Timiza Malengo, Wezesha Binti na Inclu-Cities, na mradi wa Vijana, Elimu, Malezi na Ajira (VEMA), yote yakiwapa vijana mafunzo ya ufundi stadi na stadi za ujasiriamali.
Aidha, amebainisha kuwa VETA inazingatia ubora wa mafunzo kwa kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia, kufanya tafiti za soko la ajira, kuendesha mfumo wa Uanagenzi Pacha (DATS) kwa kushirikiana na makampuni 351, na kuwajengea uwezo watumishi 479 ili kuhakikisha wahitimu wanakidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Pia ameongeza kuwa VETA inaendelea kuhamasisha wanawake kushiriki kwenye mafunzo ya ufundi stadi, huku mwaka 2025 ikiwafikia wanawake 16,000, na mwaka huu 2026 lengo likiwa ni kuwafikia wanawake 3,000, hatua inayolenga kuwawezesha kushiriki kwenye zabuni za umma kupitia makundi maalum.





