Na. John Bukuku – Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Tanzania inahitaji waandishi wake wa ndani ili kukuza vipaji vya uandishi na kuhakikisha upatikanaji wa vitabu bora vitakavyotumika mashuleni, akitaja kuwa wapo waandishi kama Profesa Penina Mlama ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika fasihi nchini.
Aidha, amebainisha kuwa kuanzishwa kwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ndani ya Taasisi ya Elimu Tanzania kunalenga kuongeza idadi ya vitabu vya ubunifu na kupanua wigo wa uchaguzi wa vitabu vinavyoweza kutumika kama vitabu vya kiada mashuleni.
Ameyasema hayo wakati akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 17, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.
Pia ameongeza kuwa kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere ni jambo la msingi kwa kuwa, licha ya kuwa mwanasiasa maarufu duniani, alikuwa mwandishi bunifu aliyekubuhu aliyeandika mashairi na tenzi nyingi hata akiwa katika majukumu mazito ya uongozi wa nchi, sambamba na kutafsiri vitabu vya falsafa na kazi maarufu za fasihi za waandishi wa kimataifa.
Amesema kuwa utoaji wa tuzo hiyo unalenga pia kuchangamsha soko la vitabu nchini, kukuza utamaduni wa kusoma na kuwajengea watoto uelewa wa utamaduni wa Tanzania kupitia vitabu vya ndani, huku Serikali ikiweka mkakati wa kununua na kusambaza vitabu vinavyoshinda mashuleni na katika maktaba ili kuongeza ushindani na ubora wa uandishi.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutenga fedha za bajeti kwa ajili ya kuendeleza tuzo hiyo, akipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kulipokea na kulisimamia kwa ufanisi ili kuhakikisha linaendelea kuwa endelevu kila mwaka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba amesema kuwa vitabu vilivyozinduliwa vitahifadhiwa katika maktaba ili wanafunzi wengi waweze kuvisoma na tayari vimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu kutumika shuleni. Aidha, amebainisha kuwa vitabu hivyo ni riwaya iitwayo Darasa, diwani ya ushairi Ngoma ya More na kitabu cha hadithi za watoto Maziwa ya Kuku, huku akieleza kuwa uchapishaji wake umefanywa na kampuni ya African Proper Education Network.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama amesema kuwa tuzo hiyo imeendelea kuwa chachu ya kukuza uandishi bunifu na utamaduni wa kusoma nchini tangu kuanzishwa kwake, akihimiza waandishi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michakato inayofuata ambayo matangazo yake yatatolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao rasmi.






