Na mwandishi wetu – Ubungo
Mnamo tarehe 17 Januari 2026, mtumishi wa DAWASA Kibamba alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kulipa faini ya Tsh 1,000,000/= na kurejesha fedha kiasi cha Tsh 297,000/= alizopokea kutoka kwa mlalamikaji kama rushwa ili arejeshe huduma ya maji aliyokuwa ameisitisha kutokana na mteja kujiunganishia maji kinyume cha taratibu (by pass).
Katika shauri Na. 15649/2025, mshtakiwa Nsajigwa Dominico Mwaipyana, ambaye ni Afisa Msaidizi DAWASA Kibamba, alishtakiwa kwa makosa mawili ya kuomba rushwa ya Tsh 300,000/= na kupokea Tsh 297,000/= kinyume na kifungu cha 15(1)(a), 2 na 3(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa SURA 329 R.E 2022 kutoka kwa mteja aliyesitishiwa huduma baada ya kujiunganishia maji kinyume na taratibu.
Mshtakiwa alipatikana na hatia kwa makosa yote mawili na kuhukumiwa kulipa faini ya Tsh 500,000/= kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, pamoja na kurejesha fedha kiasi cha Tsh 297,000/= alizopokea.
Shauri hili liliendeshwa na wanasheria Anifa Kapinga na Sophia Nyanda.
TAKUKURU Ubungo, Februari 18, 2026.





