Na. John Bukuku
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, Februari 20, 2026 amezindua na kugawa rasmi kadi za Bima ya Afya kwa Wote katika viwanja vya Dumila, wilayani Kilosa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Shaka amesema jumla ya wananchi 9,437 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo, ambao unalenga kuwawezesha kupata huduma za afya kwa urahisi na gharama nafuu. Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua kadi hizo na kuzitumia ipasavyo ili kuboresha ustawi wao na familia zao, huku akisisitiza ushirikiano kati ya wananchi na watoa huduma za afya ili kuhakikisha mpango huo unaleta matokeo chanya katika wilaya ya Kilosa.






