Na Andrea Kadege, WAF-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya Sehemu ya Uratibu wa Sekta ya Afya kwa kushirikiana na Mtaalam Mshauri (Delivery Associates) imekutana na kujadili namna ya kuendelea na utekelezaji wa afua za Uratibu wa Sekta ya Afya zinazofadhiliwa na Taasisi ya Gates Foundation.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kikichofanyika Februari 26, 2026 Mkoani Dodoma, Mkuu wa Sehemu ya Maboresho ya Sekta ya Afya Dkt. Vivian Wonanji amesema majadiliano hayo yamejikita kwenye kuendeleza ushirikiano na utekelezaji wa afua zilizo chini ya ufadhili wa Taasisi Gates Founfation.
Amesema kupitia kikao hicho wamejadili juu ya kuongeza ushirikiano wa kuboresha vipaumbele vya eneo la uzalishaji wa bidhaa za afya (Local Manufacturing) na uimarishaji wa Mfumo bora wa Afya nchini.
“Uzalishahi wa bidhaa za afya si tu ajenda ya Tanzania pekee, bali ni ya Afrika kwa ujumla huku lengo kuu ikiwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya uwezekezaji wa viwanda vya bidhaa za afya ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa dawa ambapo 80% ya dawa zinaagizwa kutoka nje ya nchi” amesema Dkt. Wonanji
Ameogeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wadau imeandaa mpango wa kukutana na idara mbalimbali zilizo chini ya sekta ya afya na kufanya ushirikishaji na kupata maoni mbalimbali yatakayosaidia kutoka na mpango madhubuti wa kuimarisha uratibu wa sekta ya afya.
Amesema kwa kuzingatia usaidizi na miongozo ya Mtaalam Mshauri (Delivery Associates) mchakato utasaidia kuandaa andiko ambalo litakwenda kufungua wigo wa Taasisi ya Gates Foundation kuwezesha Serikali moja kwa moja katika kuandaa mazingira wezeshi ya uwekezaji katika viwanda vya bidhaa za afya.




