Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar (kushoto) akiwa na Mwandishi wa vitabu vya Anatomia kutoka MUHAS, Profesa David Ngassapa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa vitabu vitano vya Anatomia katika hafla fupi iliyofanyika leo Februari 27, 2026, Dar es Salaam katika siku ya hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa (wapili kulia) akiwa na Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation Tully Esther Mwambapa (wapili kushoto) wakisaini makubaliano ya kimkakati kwa ajili ya kuimarisha ubunifu, ujasiriamali na upatikanaji wa mitaji kwa vijana hususan katika sekta ya afya.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika MUHAS leo Februari 27, 2026, Dar es Salaam katika siku ya hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS.
Mwandishi wa vitabu vya Anatomia MUHAS, Profesa David Ngassapa akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika MUHAS leo Februari 27, 2026, Dar es Salaam katika siku ya hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS iliyoenda sambamba na uzinduzi wa vitabu vitano vya Anatomia

Mkuu wa Kitengo cha Ubunifu MUHAS Dkt. Nelson Masota akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika MUHAS leo Februari 27, 2026, Dar es Salaam katika hafla ya hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, akimuwakilisha Waziri wa Elimu, pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa na viongozi wengine wa chuo akitembelea mabanda ya maonesho ya bunifu mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar (wa kwanza kushoto) akiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa na viongozi wengine wa chuo wakiwasili katika ukumbi kwa ajili ya kushiriki hafla ya hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika hafla ya kushiriki hitimisho la Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na MUHAS.
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imevitaka vyuo vya elimu ya juu nchini kuiga mfano wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika kuendeleza bunifu na kuandika vitabu, hatua itakayosaidia kuongeza uweledi na kuzalisha wahitimu bora.
Akizungumza Februari 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Wiki ya Ubunifu 2026 ya MUHAS, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, amesema serikali itaendelea kuhamasisha bunifu na kuchochea matumizi ya teknolojia ili kuleta tija kwa Taifa.
Hafla hiyo ilienda sambamba na uzinduzi wa vitabu vitano vya Anatomia pamoja na utiaji saini wa makubaliano ya kuendeleza bunifu kati ya MUHAS na CRDB Foundation.
“Wakati umefika kwa vyuo vingine kuhamasika katika kukuza bunifu pamoja na kuandika vitabu ili kusaidia jamii,” amesema Dkt. Omar, akisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za ndani katika kuandaa vitabu kama ilivyofanya MUHAS.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amewashukuru wadau kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kukuza ubunifu chuoni hapo.
Amesema kuwa baadhi ya bunifu tayari zimeanza kuingia sokoni na nyingi zimelenga kutatua changamoto za jamii, ikiwemo uchunguzi wa magonjwa na masuala ya uzazi.
Profesa Kamuhabwa amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, MUHAS imetenga shilingi bilioni 35 kwa ajili ya kusaidia bunifu.
“Asilimia 90 ya bunifu zimebuniwa na vijana ambao ni wanafunzi wetu. Tunaendelea kuwapongeza kwa kazi nzuri,” amesema.
Makubaliano kati ya MUHAS na CRDB Foundation yatadumu kwa miaka mitano, yakilenga kushirikiana katika tafiti, kutafsiri matokeo ya tafiti kuwa sera, pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa bunifu zinazolinda mazingira.
Naye Mwandishi wa vitabu vya Anatomia MUHAS, Profesa David Ngassapa, amesema vitabu hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa udaktari.
Ameeleza kuwa anatomia ni somo la msingi katika taaluma ya udaktari kwa kuwa humwezesha mwanafunzi kuuelewa mwili wa binadamu, mifumo yake na mabadiliko yanayotokea katika hatua mbalimbali za maisha.
Amefafanua kuwa vitabu hivyo vimeandaliwa kwa lugha rafiki na kuzingatia mfumo wa elimu unaolenga umahiri badala ya kukariri.
“Mitaala yetu sasa inazingatia umahiri. Huwezi kuwa na mtaala wa umahiri halafu vitabu vinazungumzia kitu kingine. Tumehakikisha vinaendana moja kwa moja na mfumo wa sasa ili mwanafunzi aelewe na aweze kutumia maarifa yake,” amesema Profesa Ngassapa.
Ameongeza kuwa gharama za kuandaa vitabu hivyo, zimetolewa na MUHAS, na kwamba chuo kina mpango wa kuvitoa pia katika mfumo wa kidijitali ili kuendana na maendeleo ya teknolojia katika elimu.
Vitabu vilivyozinduliwa ni: Human Anatomy Dissection Manual, Essentials of Human Embryology, Histology, Practical Manual on Tooth Morphology pamoja na Postnatal Growth of the Craniofacial Region and the Masticatory Apparatus
Kupitia vitabu hivi, MUHAS inaendelea kuimarisha elimu ya tiba na afya kwa kuandaa rasilimali zinazozingatia umahiri na mahitaji halisi ya wanafunzi.
Katika hafla hiyo ya kuhitimisha Wiki ya Ubunifu 2026, MUHAS pia imewatambua vijana waliofanya vizuri katika bunifu kwa kuwapatia zawadi mbalimbali kama ishara ya kuthamini mchango wao.





