Na Silivia Amandius
Kyerwa, Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe, amekabidhi rasmi nyumba kwa familia ya Ndg. Jenifer Richard, mkazi wa Kakerere, Kata ya Nkwenda, nyumba iliyojengwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Devotha Daniel Mburarugaba, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuwasaidia wananchi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, DC Msofe alimpongeza Mbunge huyo kwa kuonesha mfano wa uongozi wa vitendo unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Alisema hatua hiyo imeimarisha mshikamano, utu na upendo ndani ya jamii.
“Nawapongeza viongozi wanaotumia nafasi zao kuleta matumaini kwa wananchi. Ni wajibu wetu sote kusaidia wasiojiweza,” alisema Msofe.
Kwa upande wake, Mbunge Devotha Daniel Mburarugaba alisema alichukua hatua ya kujenga nyumba hiyo baada ya kuona picha za Jenifer kupitia mitandao ya kijamii akiwa katika mazingira magumu ya maisha.
“Niliguswa sana na hali niliyoiona. Leo tunashuhudia matokeo ya mshikamano na upendo wa kweli,” alisema Mbunge huyo.
Mbali na ujenzi wa nyumba hiyo, Mbunge ameahidi pia kuikatia familia hiyo bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha wanapata huduma za matibabu kwa uhakika na kwa wakati.
Kwa niaba ya familia, ndugu wa karibu walitoa shukrani za dhati kwa Mbunge na uongozi wa Wilaya ya Kyerwa kwa msaada huo mkubwa, wakieleza kuwa walikuwa wanaishi katika mazingira magumu kwa muda mrefu. Walisema nyumba hiyo imekuwa mwanzo mpya wa maisha yao na imewarejeshea matumaini na heshima katika jamii.
Katika hafla hiyo, Mbunge Devotha Daniel Mburarugaba alimpongeza pia Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri yanayowawezesha viongozi kuwahudumia wananchi na kusimamia maendeleo ya watu wenye mahitaji maalum.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa chama na serikali, viongozi wa dini pamoja na wananchi wa Kata ya Nkwenda waliojitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria na la kugusa mioyo ya wengi.





