Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali Ikulu, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala ya diplomasia, ushirikiano wa kimataifa pamoja na maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, Rais Dkt. Samia alikutana na Balozi wa Singapore nchini Tanzania, Mhe. Douglas Foo, na kujadili namna ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Singapore kwa manufaa ya pande zote mbili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mazungumzo hayo pia yalihusu masuala ya miundombinu, ikiwemo barabara na teknolojia ya mawasiliano, pamoja na ushirikiano katika ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wa Kitanzania hususan vijana, kwa lengo la kukuza ujuzi na kupanua fursa za ajira.
Aidha, Rais Dkt. Samia alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Inter-Parliamentary Union (IPU), Ndugu Martin Chungong, ambapo walijadili ushirikiano kati ya Tanzania na IPU pamoja na maandalizi ya Mkutano wa 153 wa IPU unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi Oktoba, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande zote mbili zilikubaliana kusimamia maandalizi ya mkutano huo kwa viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha unafanyika kwa mafanikio na kuitangaza Tanzania kimataifa. Katibu Mkuu huyo wa IPU alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa ushirikiano wa Serikali katika maandalizi ya mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wageni 2,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Rais Dkt. Samia alithibitisha utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea na maandalizi yanayokidhi vigezo vya IPU ili kuufanya mkutano huo kuwa wa mafanikio na wa kihistoria kwa nchi.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alikutana na ujumbe wa World Health Organization (WHO) ulioongozwa na Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi. Ujumbe huo ulimpongeza Rais kwa utekelezaji wa ahadi ya Bima ya Afya kwa Wote ndani ya siku 100 tangu kuanza kwa kipindi chake cha pili cha uongozi.
WHO pia ilimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuteuliwa na African Union (AU) kuwa Kinara wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, uteuzi unaotambua juhudi zake katika kuimarisha sekta ya afya nchini na maono yake kwa Bara la Afrika.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia alimpongeza Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation (DMF), Bi. Doris Mollel, kwa ujenzi wa wodi ya watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, kwa ushirikiano na taasisi ya Keep a Child Alive inayoongozwa na mwanamuziki Alicia Keys wa Marekani.
Akiunga mkono juhudi hizo, Rais Dkt. Samia alibainisha hatua zinazoendelea kutekelezwa na Serikali katika kuboresha sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya, vituo vya afya na zahanati, pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali na vituo vya afya nchini.





