NA DENIS MLOWE IRINGA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, ameongoza tamasha la michezo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 8, mwaka huu.
Akizungumza katika tamasha hilo, Mlawa amesema wanaishukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha siku hiyo kufanyika vizuri. Ameeleza kuwa wanawake wa Manispaa ya Iringa wapo katika mfululizo wa maadhimisho hayo ambayo kilele chake kitakuwa Machi 8.
Amesema maandalizi yalianza Machi 2, ambapo wanawake walifanya usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na pia walitoa vifaa mbalimbali kwa wagonjwa. Leo Machi 4, wamefanya bonanza lililohusisha jogging na michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, kukimbia na kuku, kukimbia na yai mdomoni, kupanga maji na kukimbia kwa kufumba macho.
Aidha, alisema kuwa mchezo wa netball ulihusisha timu za Chuo Kikuu cha Iringa, Mkwawa University College, Manispaa ya Iringa, TANESCO pamoja na taasisi nyingine za umma na wananchi.
Katika tamasha hilo pia kulikuwepo na ushiriki mkubwa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Mlawa amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea maadhimisho ya kilele.
Aidha, Machi 4 kulifanyika tukio maalum katika Viwanja vya Garden ambapo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kasper Kasper Mmuya alishiriki kuwapatia kina mama zaidi ya 100 hati miliki za ardhi.
Alisema kuwa Zoezi hilo lilianzishwa Machi 2 na linatarajiwa kufikia tamati Machi 7, ambapo wananchi wanaendelea kupata elimu juu ya masuala ya ardhi katika eneo la Garden.
Naibu Waziri pia alisikiliza na kujibu kero za wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi.
Kesho, Machi 5, wanawake wa Manispaa ya Iringa wataendelea na kongamano kubwa litakalofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Lugalo, ambapo mada muhimu zitatolewa kuhusu malezi ya familia, afya ya akili, ujasiriamali na utunzaji wa fedha.
Mnamo Machi 7, wanawake wa Manispaa ya Iringa watakutana katika Uwanja wa Samora ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta. Hapo kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya shughuli za wanawake, huku usiku kutafanyika Usiku wa Mwanamke wa Manispaa ya Iringa ambapo mgeni rasmi atakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bi. Dolin Sekelesa.
Mlawa amesema kuwa wanawake wa Manispaa ya Iringa wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi manispaa, na ameishukuru jamii kwa ushirikiano wao.




