
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungumza leo Machi 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa akifungua Kongamano la Magonjwa Adimu 2026 lililoandaliwa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa Kushirikiana na Taasisi ya Ali Kimara Rare Disease Foundation (AKRDF)

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS , Profesa Emmanuel Balandya, akizungumza leo Machi 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Magonjwa Adimu 2026 lililoandaliwa na MUHAS kwa Kushirikiana na AKRDF

Mwenyekiti wa AKRDF, Bi. Sharifa Mbaraka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Kongamano la Magonjwa Adimu 2026

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS , Profesa Emmanuel Balandya (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa AKRDF, Bi. Sharifa Mbaraka wakisaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kufanya tafiti kuhusu magonjwa adimu.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe (katikati), Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS , Profesa Emmanuel Balandya wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano Magonjwa Adimu 2026.

……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeingia makubaliano na Ali Kimara Disease Foundation (AKRDF) kwa kupokea shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufanya tafiti kuhusu magonjwa adimu. Huku Serikali ikiahidi kuwezesha upatikanaji wa rasilimali ili kuimarisha ukusanyaji wa takwimu sahihi, kuboresha utambuzi na kuandaa sera pamoja na miongozo inayozingatia ushahidi wa kisayansi.
Akizungumza Machi 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Magonjwa Adimu 2026 lililoandaliwa kwa ushirikiano wa MUHAS na AKRDF, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za chuo hicho kuwa kitovu cha ubora, ubunifu na utafiti kwa maendeleo ya taifa na ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameeleza kuwa MUHAS ina wajibu wa kuongoza tafiti na kuzalisha wataalamu mahiri katika sekta ya afya. Aidha, amebainisha kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za rufaa na kuimarisha mifumo ya matunzo inayounganisha huduma za msingi na za kibingwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Magembe, duniani kuna zaidi ya magonjwa adimu 7,000 yanayoathiri takribani watu milioni 400. Asilimia 80 ya magonjwa hayo husababishwa na vinasaba, na wastani wa mtu mmoja kati ya 2,000 huathirika.
Amesema kuwa nchini Tanzania, inakadiriwa kuwa asilimia sita ya wananchi wanaweza kuwa na aina fulani ya ugonjwa adimu.
Dkt. Magembe amesema kuwa miongoni mwa magonjwa adimu yanayoonekana zaidi ni selimundu, hemofilia, tawahudi, lupus erythematosus na Gaucher. Kwa ujumla, magonjwa hayo yanaathiri kati ya watu milioni tatu hadi nne, wengi wao wakiwa watoto, hali inayoonesha kuwa suala hilo ni kipaumbele cha kitaifa kinachohitaji mikakati madhubuti.
Akitoa mfano wa selimundu, Dkt. Magembe amesema huduma zake zinapatikana katika mikoa yote na zaidi ya asilimia 80 ya hospitali za wilaya, lengo ni kuhakikisha wagonjwa wanagunduliwa mapema na kupatiwa huduma jumuishi kulingana na mahitaji yao.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS , Profesa Emmanuel Balandya, amesema MUHAS inatambua jukumu lake katika utoaji wa elimu, utafiti na huduma zinazohusu magonjwa adimu.
Ametaja changamoto zilizopo kuwa ni pamoja na uhaba wa vipimo vya vinasaba, gharama kubwa za uchunguzi na utegemezi wa maabara za nje ya nchi.
Ameongeza kuwa kupitia tafiti, ubunifu na ushirikiano na wadau, chuo kinaendelea kutafuta suluhisho endelevu yatakayotekelezwa ndani ya mfumo wa afya nchini.
“Kongamano hili, limeandaliwa kama jukwaa la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuibua mapendekezo yatakayobooresha utambuzi, matibabu na ubora wa maisha ya wagonjwa. Pia litatumika kusikiliza maoni ya wagonjwa na familia zao na kujadili namna bora ya kuimarisha rufaa kuanzia ngazi ya msingi hadi huduma za juu’ amesema Profesa Balandya.
Naye Mwenyekiti wa AKRDF, Bi. Sharifa Mbaraka, amesema matokeo ya tafiti yanatarajiwa kuleta maboresho chanya kwa watoto na jamii kwa ujumla, hasa yatakapoingizwa katika sera za afya.
Ameeleza kuwa makubaliano na MUHAS yanalenga kuanzisha tafiti mahususi, akibainisha kuwa kwa sasa watoto wenye magonjwa adimu hawatambuliwi ipasavyo katika mifumo ya bima ya afya, hivyo wanahitaji msaada zaidi.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Magonjwa Adimu: Ni Zaidi ya Tunavyoweza Kufikiria,” inalenga kuhamasisha jamii kutambua suala hilo kama ajenda ya kijamii, kielimu, kiutafiti na kisera inayohitaji ushirikiano wa wadau wote.



