Afisa Ustawi wa Makao ya Watoto Kurasini, Andrew Haule akiwakaribisha wanawake wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembelea makao hayo jana jijini Dar es Salaam na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali wenye thamani ya shilingi milioni 3.55 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Theresia Marombe akisaini kitabu cha wageni wakati yeye na wanachama wa chama hicho walipotembelea Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es Salaam jana na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 3.55 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
7/3/2026 Familia zimetakiwa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano ili kuwalinda watoto dhidi ya changamoto za malezi zinazoweza kuwafanya baadhi yao kukimbilia kuishi katika mazingira hatarishi ikiwemo mitaani.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sr. Theresia Marombe wakati wanawake wa taasisi hiyo walipotembelea Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Sr. Theresia ambaye pia ni Afisa Muuguzi katika taasisi hiyo alisema migogoro ya kifamilia na hali ngumu za maisha ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watoto kukosa malezi bora na hatimaye kuishi katika mazingira hatarishi.
Alisema ni muhimu kwa wazazi na walezi hususan wanawake ambao ni nguzo ya familia kuhakikisha wanatunza na kuimarisha misingi ya familia ili kupunguza tatizo la watoto wanaoishi mitaani.
“Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, wanawake wa JKCI tumetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika makao haya ikiwemo jiko la kuoka mikate lenye thamani ya shilingi milioni 2.2 lenye uwezo wa kuoka mikate 60 kwa wakati mmoja, mchele na sukari vitu vyote hivi thamani yake ni shilingi milioni 3.55 lengo likiwa ni kusaidia kuboresha huduma kwa watoto wanaoishi katika makao haya”, alisema Sr. Theresia.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Makao ya Watoto Kurasini, Farida Kabezya aliishukuru JKCI kwa msaada huo na kuiomba jamii kujenga utamaduni wa kuwatembelea na kuwasaidia watoto wanaoishi katika makao hayo.
Alisema makao hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uzio pamoja na baadhi ya vifaa tiba kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
“Tunaishukuru sana JKCI kwa kutukumbuka na kutuletea msaada huu muhimu. Tunawaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kwani watoto wengi waliopo hapa wanasoma na wanahitaji kutiwa moyo ili kufikia ndoto zao”, alisema Farida.
Nao wanachama wa Chama cha Wanawake wa JKCI walisema wamefarijika kushiriki kuadhimisha Siku ya Wanawake kwa kuwasaidia watoto hao na kuwaletea tabasamu.
“Tunafanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa wakiwemo watoto, hivyo tunafahamu mahitaji yao ya msingi. Tumeona ni vyema katika siku hii muhimu kuwatembelea na kuwafariji watoto hawa”, alisema Afisa Muuguzi wa JKCI, Magerth Mbaruku.
“Watoto hawa wana ndoto kubwa za kuwa viongozi, madaktari, walimu na wataalamu mbalimbali wa kesho wa taifa letu. Ni wajibu wa jamii kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu kama huduma za afya, elimu bora na lishe, ili kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao na kuwa tegemeo la baadaye la nchi”, alisema Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa JKCI, CPA. Agnes Kuhenga.
Makao ya Watoto Kurasini yana jumla ya watoto 94, wakiwemo wavulana 60 na wasichana 34. Makao hayo yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Sura ya 13 Marejeo ya mwaka 2019, pamoja na kanuni zake ikiwemo Kanuni ya Makao ya Watoto ya Mwaka 2012 na kanuni za ulinzi na usalama wa mtoto.





